MENEJA wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Iringa, Mhandisi Sadiki Karume, amesema barabara ni miongoni mwa vipaumbele vikubwa katika maendeleo ya wananchi, hivyo taasisi hiyo inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha changamoto za miundombinu hiyo zinapatiwa ufumbuzi.

Akizungumza mbele ya Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, pamoja na wananchi, wa kata ya Makorongoni Mhandisi Karume amesema TARURA inatambua umuhimu wa barabara katika kufungua fursa za kiuchumi, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuwawezesha wananchi kufika katika huduma mbalimbali za kijamii.

Amesema miongoni mwa changamoto kubwa zilizowasilishwa ni pamoja na hali ya Kivuko cha Kilongo, ambacho wananchi wamekuwa wakikitaja kutokana na umuhimu wake katika usafiri na shughuli zao za kila siku.

Mhandisi Karume, alisema TARURA iko tayari kushirikiana na Mbunge Ngajilo pamoja na wananchi kuhakikisha changamoto hiyo inafanyiwa kazi kwa kuzingatia umuhimu wake kwa wananchi katika mawasiliano ya barabara
Akizungumza wakati akijibu moja ya maswali ya wananchi waliouliza kuhusu ubovu wa vivuko kwenye korongo la Kilongo amesema timu yake itafika eneo hilo kufanya tathmini ya hali halisi na kuangalia hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kupata suluhisho la kudumu.

“Hili tunalichukua kwa uzito wake. Timu yangu tutaweza kufika na kuona tatizo kubwa hili la Kilongo na kuona itatuwaje vipi changamoto ya Kilongo,” amesema Mhandisi Karume.

Aidha, Mhandisi Karume amesema eneo hilo lina vivuko kadhaa vinavyohitaji kuangaliwa, akieleza kuwa TARURA itaendelea kufanya tathmini ya mahitaji ya wananchi na kupanga hatua kulingana na vipaumbele na uwezo wa kifedha.

Kuhusu barabara nyingine zilizotajwa na wananchi kuwa zimeharibika na kuhitaji matengenezo, amesema TARURA imepokea malalamiko na mapendekezo hayo na kwamba baadhi ya barabara tayari zinafanyiwa kazi huku nyingine zikiendelea kufanyiwa tathmini.

Ametaja pia barabara ya Nyingi pamoja na barabara nyingine zilizotajwa katika mikutano ya wananchi, akisema TARURA itaendelea kuzifanyia kazi kulingana na mpango na upatikanaji wa fedha.

Mhandisi Karume amesema pale ambapo matengenezo yanahitaji fedha nyingi zaidi, TARURA inaweza kuwasilisha maombi rasmi kwa ajili ya kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema kuhusu barabara zinazopendekezwa kujengwa kwa kiwango cha lami, TARURA itaendelea kuzipokea na kuzifanyia kazi kwa kuzingatia vigezo vinavyotakiwa, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, viongozi na wananchi.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Karume amesisitiza umuhimu wa kuboresha mawasiliano kati ya TARURA na wananchi kabla na wakati wa utekelezaji wa miradi.

Amesema TARURA itaendelea kutoa taarifa kwa wananchi kabla ya kuanza kwa kazi na wakati kazi zikiendelea ili wananchi waweze kutoa maoni yao na Serikali kupata mrejesho kuhusu utekelezaji wa miradi.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kuboresha utekelezaji wa miradi na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, amekuwa akifanya ziara katika kata mbalimbali za jimbo hilo kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi, ambapo suala la barabara, vivuko na miundombinu mingine limekuwa miongoni mwa changamoto zinazowasilishwa kwake na kupatiwa majibu papo hapo na wataalamu na mengine kuyachukua kupeleka kwenye ngazi za juu