Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bw. Alban Mark Kihula, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Septemba 18, 2026, kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.
Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Wakala wa Vipimo (WMA) umewataka wananchi wanaonunua mchanga, kokoto, kifusi na mawe kuacha kununua kwa “trip” na badala yake kutumia kipimo cha cubic meter ili kuhakikisha wanapata kiasi sahihi cha bidhaa wanacholipia.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 18, 2026 jijini Dodoma, kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27. Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Bw. Alban Kihulla, amesema kuwa Wakala umeendelea kuhakiki malori yanayobeba mchanga, kokoto, kifusi na mawe ili kubaini uwezo wa kila lori kwa kipimo cha cubic meter.
Amesema kuwa baada ya lori kufanyiwa uhakiki, huandikwa pembeni uwezo wake wa kubeba kwa cubic meter, ambao unaweza kuwa 1.5, 2 au hadi 30 kwa malori yanayobeba kokoto nyingi.
Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, WMA umehakiki malori 27,282, huku akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuangalia kipimo kilichoandikwa pembeni ya lori kabla ya kununua mchanga au kokoto.
Aidha, Kihulla amesema kuwa katika kipindi hicho WMA umehakiki jumla ya vipimo 1,166,995 kati ya lengo la vipimo 1,269,957, sawa na asilimia 92 ya lengo lililowekwa.
Amesema kuwa miongoni mwa vipimo vilivyohakikiwa ni mita za maji 314,423, matenki makubwa ya kuhifadhia mafuta 286 na flow meters 2,125 zinazotumika kupima mafuta yanapokuwa yakitembea.
Pia ameongeza kuwa Wakala umehakiki tenki 16,252 zinazotumika kusafirisha mafuta, tenki 7,381 za kuhifadhia mafuta katika vituo vya mafuta pamoja na pampu 17,289 za kuuzia mafuta.
Amebainisha kuwa WMA pia umehakiki mizani 497,807 inayotumika katika maeneo mbalimbali, huku katika jukumu la ukaguzi ukifanya ukaguzi 5,015 dhidi ya lengo la 4,000, sawa na kuvuka lengo kwa asilimia 25.
Aidha, amesema kuwa Wakala ulikagua bidhaa zilizofungashwa 21,262 zinazozalishwa nchini na bidhaa 17,774 kutoka nje ya nchi, huku ukiendelea kuboresha mifumo ya kidigitali kwa ajili ya huduma za uhakiki, ukaguzi, leseni na vibali.
Ameongeza kuwa lengo la majukumu hayo ni kujenga uaminifu katika biashara, kumlinda mlaji na mtoa huduma, pamoja na kuhakikisha vipimo vinavyotumika nchini vinakuwa sahihi, huku akisisitiza kuwa kilo moja iwe kilo moja, lita moja iwe lita moja na mita moja iwe mita moja.

