Na Mwandishi Wetu, Tanga.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imewezesha ziara ya mafunzo kwa Viongozi wa Mila (Malaigwanani), Wazee Mashuhuri na kinamama 33 kutoka kata 11 za tarafa ya Ngorongoro kutembelea kiwanda cha kuzalisha na kuchakata mazao ya maziwa cha Tanga Fresh, kilichopo jijini Tanga.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Malaigwanani Ngorongoro na Diwani wa Kata ya Olbalbal, Mhe. Metui Shaudo alisema, ziara hiyo imewapa fursa ya kuona kwa vitendo hatua mbalimbali zinazofanyika katika uchakataji wa maziwa, kuanzia ukusanyaji wa maziwa, uzalishaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali zilizoongezewa thamani.

 “Tumetembelea kiwanda hiki kujifunza na kuona mambo mengi ambayo tunaweza kuyatumia tunaporudi Ngorongoro, tumeona kuwa maziwa yanaweza kuwa na thamani kubwa zaidi yakichakatwa vizuri badala ya kuuzwa yakiwa ghafi kama ambavyo mara nyingi inafanyika kwa wananchi wetu, baada ya ziara hii tutapelekeaa elimu hii kwa wananchi wenzetu ili kuwaongezea tija na kipato kinachotokana na ufugaji,” alisema Mhe. Shaudo 

Kina mama walioshiriki ziara hiyo wameelezea kufurahishwa na manufaa yanayotokana na mifugo na kuwaongezea ujuzi wa uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya mifugo na kuahidi kutoa elimu hiyo kwa wananchi wa Ngorongoro ili waendelee kujikwamua kiuchumi.

Kiongozi wa mila kutoka kata ya kakesio Ole Kotika ameeleza kuwa ziara hiyo inaendelea kuimarisha mahusiano mazuri kati ya hifadhi ya Ngorongoro na wananchi hasa kuwaongezea fursa ya kujifunza shughuli za ufugaji wa kisasa, usindikaji wa bidhaa za maziwa zenye ubora na kuongeza mnyororo wa thamani ambao unasaidia kukuza uchumi wa wananchi.

Ziara ya viongozi hao ni sehemu ya jitihada za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii ya kuwawezesha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kupata ujuzi na uzoefu unaoweza kuboresha shughuli zao za kiuchumi na kuongeza thamani ya rasilimali walizonazo.