Dodoma

‎Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE umezindua Mpango Mkakati wa Usalama Barabarani na Mpango Kazi wa Miaka Kumi (10) (2026–2036) unaolenga kupunguza vifo na majeruhi wanaotokana na ajali za barabarani.

‎Mkakati huo unaweka azma ya kuelekea Dira ya Sifuri (Vision Zero) kwa kulenga kupunguza kwa angalau asilimia 50 ya vifo na majeraha mabaya yanayotokana na ajali za barabarani katika mtandao wa barabara unaosimamiwa na TARURA ifikapo mwaka 2036.

‎Akifungua warsha ya uzinduzi wa mkakati huo jijini Dodoma Kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Naibu Katibu Mkuu,;Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bw. Sospeter Mtwale amesema mpango huo umeandaliwa kupitia mradi wa RISE na utatumika kama mwongozo wa kiutendaji katika usimamizi wa rasilimali za barabara za mikoa na wilaya.

‎Amesema mkakati huo umezingatia pia malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa hususan Lengo la 3.6 na Lengo la 11.2 pamoja na mfumo wa sera ya kimkakati na “Implementation-driven Action Plan Matrix” unaolenga kuhakikisha mipango ya usalama barabarani inatekelezwa.

‎Bw. Mtwale amesema usalama barabarani unaendelea kuwa kipaumbele cha kitaifa huku akieleza kuwa serikali inalenga kuhakikisha kunakuwa na mazingira salama ya usafiri wa barabarani yanayokidhi viwango vinavyokubalika kimataifa.

‎Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Hamidu Mataka amewataka Mameneja wa TARURA wa mikoa kutumia mkakati huo katika utekelezaji wa majukumu yao na kuhakikisha kwamba sanifu za miundombinu ya barabara inazingatia usalama wa wananchi na watumiaji wote wa barabara ikiwemo watembea kwa miguu.

‎Mhandisi Mataka pia amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kiusalama katika kipindi cha mvua ikiwemo kuhakikisha miundombinu ya barabara kama vile mitaro ya kitiririsha maji ya mvua inatunzwa ipasavyo.

‎Naye, Msimamizi Msaidizi wa mradi wa RISE, Mhandisi Lwitiko Mwandobo amesisitiza umuhimu wa kutolewa elimu kwa wadau kutoka mikoa yote na kuendelea kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara za TARURA kwani upatikanaji na uelimishaji wa mkakati huu ni moja ya majukumu yaliyopo kwenye mradi huo ambao unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na serikali ya Tanzania kupitia TARURA.

‎Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Usalama Barabarani TARURA Makao Makuu, Mhandisi Faiza Mbange amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pamoja katika kutekeleza mkakati huo akiwataka watumiaji wa barabara na taasisi nyingine zinazohusika na usalama barabarani kushirikiana katika kufikia malengo yaliyowekwa.

‎Naye, Meneja wa TARURA mkoa wa Dodoma, Mhandisi Edward Lemelo amesisitiza utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Mtendaji Mkuu ikiwemo kuhakikisha mitaro ya barabara inasafishwa ili kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara hususan wakati wa mvua za El nino.

‎Mkakati huo wa miaka 10 unalenga kuimarisha usalama wa miundombinu ya barabara na kuongeza ushirikiano miongoni mwa wadau katika jitihada za kupunguza ajali, vifo na majeraha yanayotokana na ajali za barabarani.