Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema Serikali inalenga kuhakikisha maeneo ya biashara yanatumika kwa utaratibu uliopangwa, huku wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara barabarani wakielekezwa katika maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya biashara.
Chalamila ameyasema hayo leo, Septemba 17, 2026, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, ambapo amesema hatua hiyo inalenga kuondoa biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa, ikiwemo pembezoni mwa barabara, huku wafanyabiashara wakipewa elimu na muda wa kuhamia katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya biashara.
Amesema kwa upande wa Soko la Kariakoo, Serikali inataka kutenganisha dhana ya mfanyabiashara na uuzaji wa bidhaa katika maeneo yasiyo rasmi, akisisitiza kuwa mtu anayefanya biashara ndani ya soko anapaswa kutambulika kama mfanyabiashara.
Amesema Mkuu wa Wilaya ya Ilala atakutana na wafanyabiashara wadogo ili kuwaeleza utaratibu huo na kutafuta namna ya kuwawezesha kufanya biashara ndani ya maeneo rasmi yaliyopo.
Chalamila amesema Serikali pia imewaomba wamiliki wa fremu na majengo ya biashara kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za upangishaji ili kuwapa nafasi wafanyabiashara wadogo kuingia katika maeneo rasmi ya biashara.
Amesema wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao barabarani watapewa muda wa elimu na uhamasishaji kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa, huku viongozi wa wilaya na halmashauri wakitakiwa kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya biashara yanatumika ipasavyo.
Aidha, Chalamila amesema utaratibu huo utasaidia kupunguza migogoro kati ya Serikali na wafanyabiashara, pamoja na kuboresha mwonekano wa jiji na usalama wa watumiaji wa barabara.
Amesema Serikali haitaki kumzuia mtu kufanya biashara, bali inalenga kuweka utaratibu utakaomwezesha mfanyabiashara kufanya shughuli zake katika eneo linalotambulika na kwa kuzingatia sheria.
Ameongeza kuwa katika maeneo makubwa ya biashara kama Kariakoo, Serikali inahitaji ushirikiano wa wafanyabiashara, wamiliki wa majengo na sekta binafsi ili kujenga mazingira bora ya biashara na kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa wananchi.

