*Ujenzi wafikia zaidi ya 60%
Arusha
Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imefanya ziara ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya barabara za kuingilia uwanja wa Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 60.
Akiongea mara baada ya ukaguzi huo Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Florian Kabaka ameridhika na utekelezaji wa mradi huo huku akisisitiza kasi ya utekelezaji wa kazi zisizohitaji maji mengi zikamilike kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua za El Nino zinazotarajia kuanza mwezi Oktoba.
Mhandisi Kabaka amesema ziara hiyo imelenga kujionea kwa vitendo maendeleo ya miradi mbalimbali, kukagua utekelezaji wa mikataba pamoja na kutoa ushauri kwa wahusika ili kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
“Tumetembelea miradi yote na kwa ujumla inaendelea vizuri. Nia yetu kubwa ni kujionea wenyewe maendeleo ya kazi na kusisitiza kwamba iendane na muda uliopangwa. Hatutaki kuona changamoto zinazoweza kuzuilika zikijitokeza baadaye,” amesema Mhandisi Kabaka.
Aidha, Bodi imemtaka mkandarasi kuzingatia utabiri wa hali ya hewa na kuchukua hatua mapema kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua ya El Nino.
Amesisitiza kuwa kazi zinazoweza kufanyika bila kutegemea maji mengi, ikiwemo baadhi ya kazi za udongo na madaraja zipewe kipaumbele na kukamilishwa kabla ya mvua.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema ziara hiyo imehusisha ukaguzi wa barabara zinazounganisha maeneo mbalimbali ya Uwanja wa AFCON huku lengo likiwa ni kuhakikisha mradi unakamilika ifikapo Mei, 2027.
Hata hivyo, Mhandisi Seff amemsisitiza msimamizi wa ujenzi huo Mhandisi Mshauri M/s Afrisa Consulting LTD aendelee kusimamia vizuri ili kazi zote zinazoweza kufanyika kabla ya mvua zifanyike ili kusiwepo na uharibifu.
Pia amemtaka mkandarasi M/s China Railway Constrution Engineering Group kufanya tena tathimini ya utayari wa kukabiliana na mvua za El Nino na kuwasilisha taarifa ili kuhakikisha kutokuwa na madhara wakati wa mvua zinazotarajiwa kunyesha mwezi Oktoba, 2026.

