Pemba: Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar, Ndg. Omar Ali Shehe, ameanza leo ziara ya siku nne kisiwani Pemba, inayolenga kuimarisha shughuli za chama na kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika ngazi za Mkoa na Majimbo.

Ziara hiyo imeanza katika Mkoa wa Micheweni, ambapo Naibu Katibu Mkuu amekutana na Kamati ya Uongozi ya Mkoa pamoja na viongozi wa Majimbo manne ya Wilaya ya Micheweni.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Ofisi ya Jimbo la Tumbe, viongozi wamepata fursa ya kuwasilisha taarifa za mwenendo wa shughuli za chama, pamoja na changamoto mbalimbali za kiutendaji zinazojitokeza katika maeneo yao.

Naibu Katibu Mkuu amesema ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuendelea kukijenga na kukiimarisha chama, hasa katika kipindi hiki muhimu ambacho chama kinaendelea kusubiri utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wakuu wa vyama.

Aidha, ziara hiyo inatoa fursa kwa uongozi wa juu wa chama kusikiliza kwa karibu changamoto zinazowakabili viongozi katika ngazi za Majimbo, kujadiliana namna bora ya kuzitatua, kutoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali na kuweka mazingira wezeshi kwa viongozi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Baada ya kukamilisha shughuli za Mkoa wa Micheweni, ziara hiyo itaendelea kesho katika Mkoa wa Wete, ambapo Naibu Katibu Mkuu anatarajiwa kukutana na viongozi pamoja na wanachama wa ACT Wazalendo katika maeneo mbalimbali.

Ziara hiyo itaendelea kwa siku nne katika mikoa ya kichama ya Pemba, ikiwa ni sehemu ya jitihada za uongozi wa chama kuimarisha mshikamano, utendaji na maandalizi ya hatua zinazofuata.