Mkurugenzi Mkazi wa Clinton Health Access Initiative, Esther Mtumbuka akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha. 

……………. 

Happy Lazaro,Arusha

ARUSHA: Taasisi ya Clinton Health Access Initiative (CHAI) imeeleza maeneo manne ya kipaumbele inayoshirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha huduma za afya, ikiwemo kuunga mkono uzalishaji wa hewa tiba ya oksijeni nchini, kuwajengea uwezo watoa huduma za afya na kuhakikisha upatikanaji wa nishati katika vituo vya afya.

Akizungumza kuhusu shughuli za taasisi hiyo nchini, Mkurugenzi Mkazi wa Clinton Health Access Initiative, Esther Mtumbuka, amesema CHAI imekuwa ikifanya kazi Tanzania tangu mwaka 2002 kwa kushirikiana na Serikali, hususan Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI.

Amesema eneo la kwanza ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika uzalishaji wa ndani (local manufacturing), ambapo CHAI imeunganisha suala la viwanda na huduma muhimu za afya, hususan huduma za dharura na za wagonjwa mahututi.

Mtumbuka amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya inasaidia Tanzania Oxygen Limited (TOL) kuongeza uzalishaji wa hewa tiba ya oksijeni, inayotumika kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo ya kupumua, watoto wachanga, wanawake wakati wa kujifungua pamoja na wagonjwa wenye matatizo ya mapafu.

Amesema CHAI inasaidia kiwanda hicho kwa kukipatia mtambo utakaowezesha kuongeza uzalishaji wa oksijeni hadi mara mbili ya kiwango kinachozalishwa kwa sasa. Aidha, taasisi hiyo inasaidia pia katika mfumo wa usambazaji wa oksijeni kutoka kiwandani hadi hospitalini.

“Tunasaidia takribani hospitali 16 katika eneo hili la hewa tiba ya oksijeni. Katika hospitali hizo tumesimika au tuna utaratibu wa kusimika matanki ya kuhifadhi oksijeni ili iweze kuwafikia wagonjwa,” amesema Mtumbuka.

Ameongeza kuwa katika hospitali sita kati ya hizo, CHAI imesaidia kuweka mfumo wa piping, unaowezesha oksijeni kutoka kwenye matanki kusafirishwa moja kwa moja hadi kwa mgonjwa kitandani kupitia vifaa maalumu vya kumpatia hewa tiba.

Aidha amesema katika eneo la pili ni kujenga uwezo wa watoa huduma za afya, ambapo CHAI inashirikiana na TAMISEMI kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalamu kupitia mpango wa clinical mentorship.

“Mpango huo unahusisha kuwapeleka wataalamu katika hospitali, vituo vya afya na hospitali za wilaya ili kuwajengea uwezo watoa huduma katika maeneo ya huduma za dharura, watoto wachanga na huduma za wagonjwa mahututi.”amesema Mtumbuka .

Amesema eneo jingine la kipaumbele ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha upatikanaji wa nishati katika vituo vya afya, ambapo CHAI kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI imefanya uchunguzi wa kina kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme katika vituo vya afya.

“Tumefika kwenye vituo karibu 7,000 kuelewa hali ilivyo kwenye upatikanaji wa umeme, iwe ni umeme wa gridi au vyanzo mbadala vya nishati. Baada ya hapo tumeshirikiana na wenzetu kutengeneza mpango mkakati wa miaka 10,” amesema Mtumbuka .

Kwa mujibu wa Mtumbuka amesema kuwa, mpango huo unalenga kubainisha maeneo ya kimkakati katika kuhakikisha vituo vya afya vinapata vyanzo vya uhakika vya umeme na nishati, huku ukizingatia pia changamoto za matengenezo ya miundombinu hiyo.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa mpango huo utasaidia kuboresha huduma mbalimbali za afya, ikiwemo huduma za uzazi kwa kina mama wanaofika kujifungua wakati wa usiku, huduma za chanjo zinazohitaji mnyororo wa baridi (cold chain), huduma za maabara zinazotegemea mashine zinazohitaji umeme pamoja na mifumo ya kuhifadhi na kusimamia takwimu za afya.

Mtumbuka ameongeza kuwa, hatua hizo ni sehemu ya ushirikiano mpana kati ya CHAI na Serikali katika kuhakikisha uwekezaji unaofanyika kwenye sekta ya afya unaendana na mahitaji halisi ya wananchi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma katika vituo vya afya nchini