Na Mwandishi Maalumu RS Arusha
Jumla ya wanafunzi 50, 481 wanatarajiwa kufanya mitihani ya kuhitimu darasa la saba mkoa wa Arusha, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa kwa mwaka 2026.
Akizungumza na mwandishi wetu, Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Elimu Mkoa wa Atusha, Mwl. Dkt.Vicent Kayombo amesema kuwa wanafunzi hao 50,481 waliosajiliwa kufanya mitihani ya Darasa la saba mwaka 2026, wasichana ni 26,293 na wavulana 24,188.
Amefafanua kuwa mitihani hiyo itafanyika kwa siku mbili tarehe 09 na 10 Septemba 2026, kwenye jumla ya shule za Msingi 835, zikiwa ni pamoja na shule za Serikali, mashirika ya dini na za binafsi.
“Tayari maandalizi yote yameshakamilika kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za mitihani ya Taifa, wasimamizi wote wa mitihani wamepatiwa semina elekezi ya usimamizi wa mitihani hiyo, wanafunzi wameandaliwa vema kitaaluma na kisaikolojia, hivyo sisi tunawatakia kila la kheri katika mitihani yao”. Amethibitisha Dkt.Kayombo
Hata hivyo amewasisitiza wanafunzi kuwa watumivu katika mitihani yao huku akiwasisitiza wasimamizi kuzingatia taratibu za mitihani ya Taifa na kujiepusha na aina yotote ya vitendo vilivyo kinyume na taratibu kwa kuwa, kazi wanayoifanya ni dhamama ya maisha ya wanafunzi wanaowasimamia.
Awali, Dkt.Kayombo amewatakia kila la kheri wanafunzi wote wanaofanya mtihani hiyo pamoja na kuwaombea kwa Mwenzi Mungu wapate ufaulu mzuri na hatimaye kufikia ndoto zao.
