Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesisitiza ushirikiano na viongozi na watendaji katika kutatua changamoto mbalimbali, ikiwemo migogoro ya ardhi, kwa kuzingatia haki, taratibu, kanuni na sheria ili kupata suluhu za kudumu.

Nyongo amesema mkoa unapaswa kujipanga kukabiliana na migogoro hiyo na kuhakikisha inakua ikipungua, huku akisisitiza umuhimu wa kila kiongozi na mtendaji kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria na haki.

Aidha, amesema ataendelea kuweka na kuboresha mazingira wezeshi ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi na kuhakikisha Pwani inaendelea kuwa kinara katika sekta ya viwanda na uwekezaji nchini.

Nyongo aliyasema hayo Septemba 8, 2026, wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kati yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Abubakar Mussa Kunenge, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe.

“Mkoa huu ni wa uwekezaji, dira naifahamu, Nimezunguka nje ya nchi na ndani ya nchi kutafuta wawekezaji, nimefika Mkoa wa Pwani ambao ni miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika uwekezaji, Naamini kila mmoja kwa kutambua wajibu wake, tutapiga hatua,” alisema Nyongo.

Vilevile Nyongo amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana kiuchumi ili kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Amesema pamoja na kuendelea kusukuma uwekezaji na ujenzi wa viwanda, atahakikisha mkoa unakuza uchumi kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji, ikiwemo kilimo, mifugo, utalii, uchumi wa buluu na sekta nyingine.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Abubakar Mussa Kunenge, amewashukuru wananchi, viongozi, watumishi na watendaji wa Mkoa wa Pwani kwa ushirikiano waliompa tangu mwaka 2021.

“Msiamini katika kushindwa, natoa wito muendelee kuchapa kazi na kuwa wamoja ili Mkoa wa Pwani upige hatua zaidi,” anaeleza Kunenge.

Akitoa neno la shukran Shangwe Twamala alisema, Kunenge alikuwa mwalimu wao na kumshukuru kwa mchango wake, huku akiahidi kwa niaba ya menejimenti ya mkoa kuendeleza ushirikiano huo katika kutekeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.