Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam 

Vijana nchini wameelezwa kuwa wanaweza kutumia taka kama chanzo cha ajira na kipato, huku Chuo cha VETA Dar es Salaam kikitarajia kuanza mafunzo maalumu ya urejelezaji taka (recycling) kuanzia Oktoba mwaka huu.

Hatua hiyo inalenga kuwajengea vijana ujuzi wa kutambua, kuchambua na kuchakata taka za aina mbalimbali na kuzibadilisha kuwa bidhaa na fursa za kiuchumi, sambamba na kusaidia kupunguza changamoto ya taka katika jamii.

Hayo yamesemwa leo Septemba 8,2026 Jijini Dar es salaam na Mkuu wa Chuo cha VETA Dar es Salaam, Abraham Puguni, baada ya chuo hicho kufanya majadiliano na wadau mbalimbali kuhusu namna bora ya kutekeleza mtaala wa mafunzo ya usimamizi wa taka na urejelezaji, ambapo VETA Dar es Salaam imechaguliwa kuwa moja ya vyuo vya majaribio (pilot) vya programu hiyo.

Alisema VETA Dar es Salaam imechaguliwa kuwa miongoni mwa vyuo vya majaribio vya programu hiyo, ambayo pia inalenga kuwafikia wananchi wanaojihusisha na ukusanyaji, uchambuzi na uchakataji wa taka pamoja na jamii inayozalisha taka.

“Wazalishaji wakubwa wa taka ni jamii kwa ujumla. Kwa hiyo mafunzo haya si kwa wale wanaochakata, kuchambua au kubeba taka pekee, bali ni muhimu pia kwa jamii inayozalisha taka,” alisema Puguni.

Alisema wahusika wa shughuli za taka watapatiwa elimu ya namna ya kufanya kazi hizo kwa kuzingatia afya na usalama kazini,huku wahitimu wakitarajiwa kupata vyeti na ujuzi utakaowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Puguni aliwataka viongozi wa mitaa na kata kushirikiana na VETA katika kutambua wananchi watakaonufaika na mafunzo hayo, akisisitiza kuwa ushiriki wa serikali za mitaa ni muhimu katika kufanikisha programu hiyo.

Kwa upande wake, Afisa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Jackline Wikechi, alisema mpango huo unaweza kusaidia kubadili mtazamo wa jamii kuhusu taka, ambazo mara nyingi zimekuwa zikionekana kama uchafu badala ya rasilimali yenye thamani.

Alisema NEMC haiwezi kukabiliana na changamoto ya taka peke yake, hivyo ushirikiano na taasisi za mafunzo kama VETA ni muhimu katika kuwajengea vijana uwezo wa kuzitambua, kuzichambua na kuzichakata taka kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.

“Naomba Watanzania waweze kuziona taka kama fursa, yaani ni kazi ambayo ni sawa na kazi nyingine, badala ya kuzidharau kwa sababu tu zinaitwa taka, Taka zinaweza kugeuka kuwa ajira ya kudumu, zikampa mtu heshima na kipato,” alisema Wikechi.

Naye Afisa Afya wa Kata ya Keko, Haji Hatibu Kikwacha, alisema anaunga mkono programu hiyo kutokana na changamoto ya taka inayoendelea katika mitaa, akieleza kuwa elimu ya urejelezaji inaweza kusaidia kupunguza taka zinazobaki bila kutumika.

Alisema viongozi wa mitaa wako tayari kushirikiana na VETA kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya wananchi, ili kuwawezesha kuelewa umuhimu wa kuchambua na kurejeleza taka zinazoweza kutumika tena.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Magulumbasi A, Kata ya Keko, Hamis Nyanza, alisema elimu hiyo imemsaidia kubadili mtazamo kuhusu taka na kuahidi kushirikiana na VETA kuwahamasisha wananchi kushiriki katika mpango huo, huku akisisitiza kuwa taka zinaweza kuwa sehemu ya fursa za kiuchumi kwa jamii.