📍 Dodoma

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuhakikisha inaweka mfumo bora na wenye ufanisi wa udahili na usajili wa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu, ili kuepusha vyuo kupokea wanafunzi wanaozidi uwezo wa miundombinu na wakufunzi waliopo na hivyo kulinda ubora wa elimu.

Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo leo, Septemba 5, 2026, jijini Dodoma, baada ya kukutana na Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu pamoja na Wenyeviti wa Mabaraza ya vyuo vikuu nchini, katika kikao kilichojadili masuala mbalimbali yanayohusu elimu ya juu, hususan mchakato wa udahili na usajili wa wanafunzi. Amesema lengo ni kuweka utaratibu utakaowawezesha wanafunzi kupata nafasi za masomo kwa haki na kwa ufanisi, huku ukizingatia uwezo halisi wa kila chuo.

“Tumefanya hivyo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunatengeneza mfumo mzuri ambao hautaleta utata, hautakuwa na kuweka idadi ya wanafunzi kuliko uwezo wa kufundisha,” amesema Prof. Mkenda,

Waziri Mkenda amewahimiza wanafunzi wanaoomba kujiunga na vyuo vikuu kuendelea kufanya maombi yao huku wakisubiri maelekezo zaidi kutoka TCU kuhusu utaratibu wa udahili. Amesema mfumo unaoandaliwa unalenga kulinda maslahi ya wanafunzi na vyuo, sambamba na kuhakikisha mchakato wa udahili unakuwa wa wazi, rahisi na wenye ufanisi.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuongeza uwezo wa vyuo vikuu nchini kupitia ujenzi na upanuzi wa kampasi katika mikoa mbalimbali, hatua inayolenga kuongeza nafasi za wanafunzi kupata elimu ya juu. Amesema uwekezaji huo utawezesha kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata fursa za elimu ya juu bila kushusha viwango vya elimu vinavyotolewa.

Profesa Mkenda amesema Tanzania bado haijafikia kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi katika elimu ya juu kinacholengwa, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na vyuo vikuu kuongeza nafasi za masomo huku ikihakikisha ubora unaendelea kuwa kipaumbele. Amesema Serikali inalenga kuwa na mfumo wa elimu ya juu unaoweza kutoa fursa zaidi kwa vijana sambamba na kuwaandaa kwa mahitaji ya soko la ajira.

Ameongeza kuwa Wizara imepanga kufanya kikao kama hicho na viongozi wa vyuo vya kati vilivyo chini ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), kwa ajili ya kujadili masuala ya ubora wa elimu, udahili na mifumo ya uongozi katika sekta hiyo. Amesema ushirikiano kati ya Serikali, vyuo na wadau wengine ni muhimu katika kuhakikisha uwekezaji unaofanywa katika elimu unazaa matokeo yanayotarajiwa.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, amesema kikao hicho kimejadili masuala mbalimbali yanayohusu udahili wa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu, ubora wa elimu pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuendeleza sekta hiyo.

Amesema wadau hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika kuboresha mifumo ya udahili, huku wakizingatia mahitaji na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya elimu.

Prof. Kihampa amesema ongezeko linalotarajiwa la wanafunzi kutokana na mabadiliko mbalimbali ya sera linahitaji Serikali, TCU na vyuo vikuu kujiandaa mapema ili kuongeza uwezo wa kutoa elimu bora kwa idadi kubwa ya wanafunzi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Teolojia cha Lweru, Aggrey Mlimuka, amesisitiza umuhimu wa vyuo vikuu nchini kusimamia ubora wa elimu ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na uwezo na weledi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Amesema vyuo vina wajibu wa kuhakikisha kila taaluma inazalisha wataalamu wenye uwezo, huku akibainisha kuwa endapo vyuo vitashindwa kusimamia ubora, soko la ajira lenyewe litachuja wahitimu kulingana na uwezo wao.

Awali Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Prof. Alfred Sife, amesema vyuo vikuu nchini vimekubaliana kuendelea kuboresha mchakato wa udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2026/2027 ili kuhakikisha wanafunzi wanaopokelewa wanakidhi vigezo na kujiunga na programu zinazolingana na taratibu, kanuni na sheria zilizowekwa.

Amesema mjadala mkubwa katika kikao hicho ulihusu mwenendo wa udahili unaoendelea kwa sasa, ambapo dirisha la kwanza la maombi limekamilika na kinatarajiwa kufunguliwa dirisha la pili wiki ijayo.

Kwa mujibu wa Profesa Sife, lengo ni kuhakikisha mfumo wa udahili unaendelea kuimarishwa ili kupata wanafunzi wenye sifa na kuwawezesha kujiunga na programu na vyuo vinavyokidhi mahitaji yao, huku taratibu, kanuni na sheria za udahili zikizingatiwa.

Aidha, Profesa Sife amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha vyuo vikuu vinaendelea kuboresha ubora wa elimu katika programu mbalimbali na kutoa wahitimu wenye uwezo unaokidhi mahitaji ya taifa na soko la ajira.