Mkurugenzi wa shule za Intels pre ,primary na sekondari ,Alexander Samson akizungumza kwenye mahafali hayo jijini Arus Mwandishi mwandamizi wa vitabu mbalimbali ,Joramu Nkumbi akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha

Happy Lazaro, Arusha.

Arusha .VIJANA nchini wametakiwa kuacha mtazamo wa kusubiri kuwa “Taifa la kesho” na badala yake kuchukua hatua sasa kwa kutumia elimu, vipaji, maarifa na uwezo walionao katika kuleta mabadiliko katika familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na mgenirasmi ambaye ni ,Mwandishi mwandamizi wa vitabu mbalimbali ,Joramu Nkumbi katika mahafali ya shule za Intels ambapo kwa upande wa kidato cha 4 ni mahafali ya 8 na mahafali ya 20 darasa la saba .

 Nkumbi amesema vijana ni sehemu muhimu ya Taifa la leo na kesho, hivyo wanapaswa kujiamini, kuthubutu kufanya mambo makubwa, kuzungumza na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili badala ya kusubiri nafasi kutoka kwa wengine.

“Vijana ni taifa la leo, lakini pia ni taifa la kesho. Vijana ni viongozi wa sasa na viongozi wa kesho. Kwa hiyo kijana, amka, jinyanyue, zungumza na fanya mambo makubwa,” amesema Nkumbi.

Amesema kuwa , hatua ya kwanza kwa kijana anayetamani kufanikiwa ni kujielimisha, akieleza kuwa elimu humsaidia kuongeza uelewa, maarifa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika maisha.

 Akimnukuu Hayati Mwalimu Julius Nyerere, amesema, “The more you know, the more you get enlightened,” akimaanisha kuwa kadiri mtu anavyopata maarifa zaidi, ndivyo anavyoongeza uelewa na mwanga wa maisha.

Amesema Mwalimu Nyerere aliwahi kufananisha vijana wanaopewa elimu na mtu anayesafiri kutoka kijiji chenye njaa kwenda mjini kutafuta chakula kwa ajili ya wananchi waliobaki kijijini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shule za Intels pre ,primary na sekondari ,Alexander Samson amesema kuwa,shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma ambapo kila mwaka wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mitihani yao

Alexander amesema kuwa,katika kuonyesha umuhimu wa kusaidia vijana na watoto kupata elimu, uongozi wa shule hiyo umeeleza kuwa kwa sasa inawasaidia wanafunzi 72 ambao hawalipi ada kutokana na changamoto za kifedha za familia zao.

 Ameongeza kuwa, wanafunzi hao huchanganywa na wenzao wanaolipa ada ili kuzuia ubaguzi na kuhakikisha wote wanajisikia kuwa sehemu sawa ya jamii ya shule.

” katika manunuzi ya chakula, wanafunzi wanaolipiwa na wale wanaolipa ada hawatenganishwi, bali shule hununua mahitaji kwa pamoja na kwa wingi, ikiwemo mahindi na maharage, ili kupunguza gharama na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata huduma sawa.”amesema Alexander 

“Wale wote ambao wanalipa tunapofanya shopping tunawachanganya, kwa sababu hatutaki ubaguzi kwa watoto na watoto wenyewe hawajui nani analipiwa na nani halipiwi kwani wote wanakaa pamoja darasani na wanaishi kama wanafunzi wengine,” amesema.

Amesema kwa kila mwanafunzi anayesaidiwa, shule hutumia takribani shilingi milioni 1.8 kwa mwaka ,hivyo kwa wanafunzi 72 gharama hiyo ni kubwa na inahitaji nguvu za pamoja kutoka kwa shule na wadau mbalimbali.

Aidha ametoa wito kwa wafadhili, wazazi na wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia, ili kupunguza mzigo wa gharama unaobebwa na shule na kuiwezesha kuendelea kuwasaidia watoto kutoka familia zenye changamoto za kiuchumi kupata elimu na malezi bora.

Amesema ushirikiano wa wadau ni muhimu kwa sababu utawezesha shule kuendelea kutoa fursa kwa watoto wengi zaidi, huku akisisitiza kuwa elimu inayotolewa kwa kijana haipaswi kubaki kwake binafsi, bali inapaswa kuwa chachu ya maendeleo kwa familia, jamii na Taifa.

Nao wahitimu wa kidato.cha nne shuleni hapo ,wamesema kuwa elimu waliyoipata imewajengea ujasiri wa kujitambua,kufikiri ,kujiamini na kufanya kazi kwa bidii sambamba na kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo elimu ya usalama katika mazingira ikiwemo elimu ya jinsia,kilimo,ufugaji,michezo ,kujitegemea ,Tehama ,Siasa ,Haki na wajibu. 

Aidha ametaja changamoto wanazokabiliana nazo ni baadhi ya wazazi kutolipa ada kwa wakati ila kutokana na changamoto hiyo shule iliweza kuwavumilia katika kipindi hicho chote .

“Kutokana na ongezeko la utandawazi katika dunia yetu sasa,tunashauri wazazi kuwa karibu na sisi ili waweze kutolea vyema na kutuelekeza katika njia iliyo bora ili tuweze kushinda vishawishi na kufikia malengo yetu na kupata elimu na malezi bora.”wamesema wahitimu hao.