Shekh Hassan Kabeke akionesha zawadi baada ya kukabdhiwa na Sheikh wa TIC Hemed Jalala (kula).

Shekh Mkuu wa TIC Hemed Jalala, akizungumza na waislamu (Picha na Baltazar Mashaka)
……….
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SHEIKH Mkuu wa Jumuiya ya Ithna Asheriyyah Tanzania (TIC), Maulana Hemed Jalala, amewataka wazazi, walezi na viongozi wa dini kuwalea vijana katika maadili mema, uzalendo, upendo na kuvumiliana ili kulinda amani na utulivu nchini.
Sheikh Jalala alisema hayo jana usiku, wakati akizungumza katika Maulid iliyowakutanisha waumini wa madhehebu na makabila mbalimbali jijini Mwanza, akisisitiza kuwa malezi bora ya vijana ndiyo msingi wa kujenga jamii yenye maadili na taifa lenye amani.
Alisema mfano bora wa kuigwa katika maadili na tabia njema ni Mtume Muhammad (S.A.W), ambaye Mwenyezi Mungu alimleta kuwa rehema kwa walimwengu wote, akirejea Qur’an, Surat Al-Anbiya, Aya ya 107 (21:107).
Aliwapongeza Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hassan Kabeke, pamoja na Sheikh wa TIC Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hashimu Ramadhan, kwa kuandaa Maulid hiyo iliyowakutanisha watu wa makabila, rangi na madhehebu tofauti.
“Umuhimu wa maadili katika hadhara hii iliyoandaliwa na kukusanya watu wa madhehebu na makabila tofauti ni jambo la kupongezwa. Haya ndiyo mafunzo ya Mtume,” alisema.
Akizungumzia malezi ya vijana, Sheikh Jalala alisema mapambano dhidi ya maovu huanzia ndani ya nafsi ya mwanadamu, akirejea mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W) kuhusu umuhimu wa kupambana na nafsi na kuikuza katika maadili mema.
“Jihad kubwa ni mafunzo makubwa ya kuwafunza maadili vijana. Hakuna kikubwa kama kupenda nchi yetu. Vijana ndiyo wanaofunzwa na kudanganywa kuharibu nchi zao, mila zao, nchi na mataifa yao,” alisema.
Alisema vijana wanapaswa kufundishwa kuipenda nchi yao na kutumia tofauti za makabila, lugha, rangi na dini kama fursa ya kujenga umoja badala ya kuzitumia kama chanzo cha migawanyiko katika jamii.
“Kwa vile sisi Watanzania ni watu wa makabila, lugha, rangi, dini na tabia tofauti, tunatakiwa kuwalea vijana katika maadili. Pia kuishi kwa amani, kuhakikisha amani na utulivu unadumu, kuelewana na kusikilizana. Huo ndiyo muonekano wa dini yetu,” alieleza.
Aidha, Sheikh Jalala aliwataka waumini kuwa na uvumilivu na kuheshimu tofauti za madhehebu, akisema tofauti hizo hazipaswi kuwa chanzo cha migogoro na hatuwezi kumbadilisha Sheikh Kabeke kuwa Shia ama Sheikh Hashim kuwa Sunni.
Alisisitiza viongozi wa dini kutumia hekima, busara na lugha nzuri katika mahubiri yao, akirejea kisa cha Nabii Musa na Haruni walipotumwa kwa Firauni, akisema somo hilo lina umuhimu katika kuwalea vijana na kujenga jamii yenye maadili.
Katika hatua nyingine, Sheikh Jalala aliwataka waumini wa madhehebu ya Shia waliohudhuria Maulid hiyo yenye kaulimbiu ‘Mtume Muhammad S.A.W; Mwongozo wa Amani, Uadilifu na Upendo katika Jamii’, kumuombea Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi ya maendeleo anayoifanya nchini.
Pia, kumuomba Mwenyezi Mungu kuilinda na kuiepusha Tanzania dhidi ya majanga mbalimbali, likiwamo tishio la El-Nino, ili amani na utulivu viendelee kudumu.
