NESTORY Mbilinyi na Joyce Oscar wamefunga ndoa takatifu, katika ibada iliyofanyika jana, Septemba 4, 2026, katika Kanisa la St. Maria De Mathias, Mivumoni, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kilele cha safari yao ya kuelekea katika maisha ya ndoa.
Ibada hiyo ya Ndoa Takatifu ilianza saa 9:00 mchana, kabla ya maharusi hao kuendelea na sherehe katika JC Hall Africana, Mbezi Beach, kuanzia saa 12:00 jioni, ambapo ndugu, jamaa, marafiki na viongozi walishiriki katika kuwapongeza na kusherehekea pamoja nao.
Baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo, familia ya Mbilinyi imetoa shukrani kwa wote walioshiriki katika maandalizi na kufanikisha Ndoa Takatifu na Harusi hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya familia yake ndogo na familia pana ya Mbilinyi, Erasmo Mbilinyi amewashukuru ndugu, jamaa, marafiki na viongozi kwa michango yao na ushiriki wao, akisema wameonesha upendo mkubwa na wa dhati kwa familia.
Erasmo amewapongeza pia viongozi wa kamati ya maandalizi kwa uratibu wa shughuli hiyo, akisema namna walivyoendesha vikao vya maandalizi mtandaoni ilikuwa ya kiwango cha juu.
“Sisi hatuna neno zuri zaidi la kushukuru zaidi ya kusema Tuhongidze,” amesema Erasmo.
Ameahidi kuwa familia yake itaendelea kushiriki kikamilifu katika matukio ya ndugu na marafiki, katika nyakati za shida na raha, huku akiwaomba wawajulishe wanapokuwa na matukio ili nao waweze kushiriki.

