📍DODOMA

SERIKALI imeendelea kuimarisha miundombinu ya umeme kwa ajili ya kuchochea uwekezaji na kuongeza uzalishaji nchini, baada ya kusainiwa kwa mkataba wa utekelezaji wa Mradi wa Mpomvu–Geita Gold Mining (GGM) wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 na ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme katika eneo la GGM

Akizungumza leo Septemba 3,2026 jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini mkataba huo, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 63.2 unalenga kuhakikisha GGM inapata umeme wa uhakika, wa kutosha na unaoaminika kwa ajili ya kuendesha shughuli zake za uzalishaji.

Amesema nishati ni msingi wa uzalishaji na kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi, hivyo Serikali itaendelea kuwekeza katika kuongeza uwezo wa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, pamoja na kuimarisha miundombinu ya kuwaunganisha wateja wakubwa kwenye Gridi ya Taifa.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, mradi huo utahusisha ujenzi wa njia ya usafirishaji wa umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Mpomvu hadi GGM yenye urefu wa kilomita 6.65, pamoja na kituo kipya cha kupokea na kupoza umeme cha 220/33kV chenye transfoma moja yenye uwezo wa MVA 90 katika eneo la mgodi huo.

“Mradi huo utatekelezwa na ubia wa kampuni za Sihotech Engineering Company na Sieyuan Electric Company Limited, huku akilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na mkandarasi kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa wakati, kwa kuzingatia viwango vya ubora, usalama na thamani ya fedha.”amesema Mhe.Makamba

Makamba amesema mradi huo ni sehemu ya mpango wa TANESCO unaohusisha miradi ya kuwaunganisha wateja wakubwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa, ikiwemo miradi ya usafirishaji wa umeme katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji madini. Alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali kuhakikisha nishati inakuwa kichocheo cha uwekezaji na uzalishaji.

Aidha, ameeleza kuwa hatua hiyo inafuatia mafanikio yaliyopatikana baada ya GGM kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa mwaka 2024, ambapo kituo cha kupokea na kupoza umeme chenye uwezo wa megawati 34 kilizinduliwa. Hatua hiyo iliwezesha mgodi kupunguza utegemezi wa umeme unaozalishwa kwa mafuta na kupunguza gharama za uendeshaji.

Amesema kabla ya kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, GGM ilikuwa ikitumia kati ya Sh bilioni 10 na 13.4 kwa mwezi kwa ajili ya gharama za umeme unaozalishwa kwa mafuta, huku matumizi ya umeme kutoka Gridi ya Taifa yakiongeza mapato ya TANESCO kwa kati ya Sh bilioni mbili na tatu kwa mwezi.

Makamba amesema Serikali pia imechukua hatua za kuimarisha uwezo wa kifedha na kiutendaji wa TANESCO ili iweze kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati. Alisema Wizara ya Fedha iliidhinisha TANESCO kukopa Sh bilioni 229.3 kutoka benki za ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya umeme unalenga zaidi ya upatikanaji wa nishati, kwani unasaidia kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza ajira na mapato, pamoja na kuvutia wawekezaji zaidi nchini.

Makamba ameipongeza TANESCO, GGM na wadau wote waliohusika kufanikisha mradi huo,huku akisema Serikali inatarajia mradi huo kukamilika ndani ya miezi 18 kama ilivyopangwa na kutoa huduma kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya uzalishaji na uwekezaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema mradi huo unatekelezwa kwa miezi 18 kutoka tarehe ya utiaji saini mkataba ukilenga kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme kwa GGM.

“Mradi huu unagharimu takribani Shilingi bilioni 63.19 za Kitanzania na kutokana na kuwa GGM ni miongoni mwa wateja wetu wakubwa wenye kuchangia kiasi kikubwa cha mapato kwa Shirika, tutahakikisha mradi huu unafanikiwa kama inavyotarajiwa kukidhi ongezeko la mahitaji yao kwa manufaa ya pande zote mbili na pato la Taifa kwa ujumla,” amesema Bw. Twange.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO kwa namna inavyosimamia Shirika katika ujenzi wa uchumi wa kisasa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Niipongeze Bodi ya Wakurugenzi TANESCO kwa namna mnavyosimamia Shirika hili kujenga uchumi wa kisasa kuelekea Dira 2050. Utekelezaji wa mradi huu unatupa nguvu zaidi kwa sababu sekta zote, nishati na madini, zipo chini yetu,” amesema Mhe. Mgalu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashimu Komba, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo amesema Uongozi wa Mkoa umejipanga kushirikiana na mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha utekelezaji wake haupati kikwazo, akisisitiza umuhimu wa nishati ya umeme katika kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali.

“Ni dhahiri, nishati ya umeme inachagiza maendeleo ya sekta zote. Tunampongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyosukuma kwa dhati agenda ya nishati ya umeme kuwafikia wananchi. Mamlaka ya Mkoa imejipanga kushirikiana na Mkandarasi wa mradi wa umeme wa Mpomvu–GGM kuhakikisha mradi haupati kikwazo,” amesisitiza Mhe. Komba.

Awali Mwakilishi wa GGM, Mhandisi Maftah Seif, amesema mradi huo utasaidia kutatua changamoto kuu mbili, ikiwemo ubora wa nishati ya umeme, ambao umekuwa ukikumbwa na mabadiliko, pamoja na ongezeko la mahitaji ya umeme linalotokana na kuongezeka kwa shughuli za uchimbaji madini.

Amesema kadri shughuli za uchimbaji zinavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya nishati yanavyoongezeka, hivyo wamekuwa wakishirikiana na TANESCO kutafuta namna ya kuongeza uwezo wa upatikanaji wa umeme na kuhakikisha uzalishaji unaendelea bila changamoto.

Aidha, amewashukuru TANESCO kwa ushirikiano, akisisitiza umuhimu wa kuangalia gharama za uwekezaji kwa mtazamo mpana, kwani wawekezaji wanapolazimika kuongeza gharama mara kwa mara baada ya kufanya uwekezaji mkubwa, hali hiyo inaweza kuwa changamoto katika uendeshaji wa miradi.