Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam.
Watoto wenye umri chini ya miaka mitano uathirika zaidi na ugonjwa wa misuli ya moyo unaojulikana kitaalamu kama Dilated Cardiomyopathy (DCM), huku historia ya maambukizi ya misuli ya moyo (myocarditis) ikitajwa kuwa sababu inayoongoza miongoni mwa sababu zilizobainika.
Hayo yamebainishwa katika utafiti uliofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Januari 2021 hadi Desemba 2025 uliangalia taarifa za watoto waliolazwa JKCI wakiwa na ugonjwa huo kwa lengo la kuchambua sifa za ugonjwa pamoja na matokeo ya matibabu yake.
Kwa mujibu wa utafiti huo, jumla ya watoto 3,330 waliolazwa JKCI katika kipindi hicho watoto 45 sawa na asilimia 1.4, waligundulika kuwa na tatizo la DCM, Hata hivyo watoto 10 waliondolewa katika utafiti kutokana na kutokamilika kwa taarifa zao za kitabibu hivyo utafiti kujumuisha watoto 35.
Akizungumzia utafiti huo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto aliyefanya utafiti huo Zawadi Kalezi alisema matokeo yameonesha kuwa kati ya watoto 35 waliofanyiwa uchunguzi, 24 sawa na asilimia 68.6 walikuwa chini ya umri wa miaka mitano, huku wavulana wakiwa wengi kwa asilimia 51.4.
Dkt. Zawadi alisema utafiti ulibaini kuwa hali ya kuvimba kwa misuli ya moyo (myocarditis) ilikuwa sababu iliyobainika mara nyingi zaidi ikihusisha watoto 15 sawa na asilimia 42.9 huku sababu nyingine kuwa hitilafu za mpangilio wa mapigo ya moyo (arrhythmias) iliyohusisha watoto watano sawa na asilimia 14.3 na watoto wengine 14 sawa na asilimia 40 chanzo cha ugonjwa huo hakikuweza kubainika.
“Utafiti umeonesha kuwa kiwango cha wastani cha uwezo wa moyo kusukuma damu (LVEF) kilikuwa asilimia 30 ikionesha udhaifu mkubwa wa kazi ya moyo kwa watoto hao”, alisema Dkt. Zawadi
Dkt. Zawadi alisema utafiti umeonesha kuwa matibabu yalisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza dalili za kushindwa kufanya kazi kwa moyo ambapo watoto 32 sawa na asilimia 91.4 walionesha kuimarika na kutokuwa tena na dalili za kushindwa kufanya kazi kwa moyo wakati wa kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Dkt. Zawadi alisema baada ya watoto hao kuruhusiwa kutoka hospitalini, wataalamu waliendelea kuwafuatilia kwa kipindi cha miezi 18 ambapo watoto saba sawa na asilimia 25 walirejea katika hali ya kawaida ya utendaji wa moyo. Watoto 11 sawa na asilimia 39.3, walionesha kuimarika kwa utendaji wa moyo, wakati watoto 10 sawa na asilimia 35.7, hawakuonesha mabadiliko katika kiwango cha utendaji kazi wa moyo.
“Utafiti umeonesha kuwa ugonjwa huo unaweza kuwa na madhara makubwa kwani watoto watano sawa na asilimia 14.3 walipata matatizo wakati wanalazwa ambapo wawili walipata kiharusi na watatu walipata tatizo la ghafla la figo, aidha watoto watano walirudi hospitalini kutokana na moyo kushindwa tena kufanya kazi vizuri”, alisema Dkt. Zawadi
Watafiti wameeleza kuwa idadi kubwa ya watoto ambao chanzo cha DCM hakikubainika inaonesha umuhimu wa kuimarisha uwezo wa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa watoto hususan vipimo vya vinasaba (genetic testing) na MRI ya moyo, ambavyo vinaweza kusaidia kubaini chanzo cha ugonjwa kwa watoto ambao sababu zake hazijulikani.
Utafiti huo uliochapishwa mwezi Agosti 2026 katika jarida la Frontiers in Cardiovascular Medicine unatoa picha ya hali ya ugonjwa wa DCM kwa watoto wanaopatiwa huduma katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) nchini na unaonesha umuhimu wa utambuzi wa mapema, matibabu na ufuatiliaji wa karibu wa watoto wenye matatizo ya moyo.