Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amesema VETA imeweka mkakati wa kuongeza udahili wa wanafunzi na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi nchini.Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 04, 2026 Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27, amebainisha kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata fursa ya kujifunza ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kujiajiri.

CPA Kasore amesema udahili wa wanachuo katika vyuo vinavyomilikiwa na VETA umeongezeka kutoka wanachuo 69,347 mwaka 2022/2023 hadi kufikia 116,468 mwaka 2025/2026.Amebainisha kuwa ongezeko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuanza kwa shughuli za vyuo vipya 33 vya VETA katika ngazi za mikoa na wilaya.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa vyuo vipya 65 vya VETA, ambavyo vinajumuisha vyuo 64 vya wilaya na chuo kimoja cha Mkoa wa Songwe, vinavyotarajiwa kuanza kutoa mafunzo Januari 2027.

Amesema kuanza kwa mafunzo katika vyuo hivyo kutapanua zaidi fursa za elimu ya ufundi stadi, ambapo jumla ya wanafunzi wapya 130,892 wanatarajiwa kudahiliwa mwaka 2027.

“Lengo letu si kuwa na majengo mapya pekee, bali kuwa na vituo hai vya ukuzaji ujuzi, ajira, kujiajiri, ubunifu, uzalishaji na maendeleo ya uchumi wa maeneo husika,” amesema CPA Kasore 

Kwa upande wa TEHAMA, CPA Kasore amesema VETA imeweka mkazo katika matumizi ya teknolojia za kidigitali ili kuongeza ufanisi na kupanua upatikanaji wa mafunzo kwa wanafunzi na wananchi.

Amebainisha kuwa kupitia Programu ya Elimu na Ujuzi kwa Ajira zenye Tija Awamu ya Pili (ESPJ II), VETA itaanzisha Jukwaa la Kitaifa la Mafunzo ya Ufundi Stadi Kidigitali (National TVET E-Learning Platform) pamoja na kuandaa moduli 50 za mafunzo mtandaoni.

Ameongeza kuwa wakufunzi na wanafunzi 250 watajengewa uwezo wa kuandaa na kuendesha mafunzo kidigitali, huku wanafunzi 8,333 wakielekezwa namna ya kujifunza kupitia mfumo huo.

“Teknolojia haitachukua nafasi ya mkufunzi, lakini itapanua uwezo wa mkufunzi kufundisha na wa mwanafunzi kujifunza,” amesema CPA Kasore 

Amesema matumizi ya TEHAMA yataenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika vyuo vya VETA, ili wanafunzi wapate mafunzo yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.

Aidha, amebainisha kuwa VETA imeendelea kuboresha mitaala ili iendane na mahitaji ya soko, ambapo mitaala mipya 29 imeandaliwa, mitaala 91 imefanyiwa mapitio na mitaala 13 imeboreshwa.

Ameongeza kuwa hatua hizo zinalenga kuhakikisha ongezeko la udahili linaenda sambamba na ubora wa mafunzo, umahiri wa wahitimu, ajira, kujiajiri pamoja na kuongeza tija na uzalishaji nchini.

Aidha, amebainisha Kuwa VETA  itaendelea kuongeza ushirikiano na waajiri, viwanda, sekta binafsi na mafundi mahiri ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia.

Amesema mkakati huo ni sehemu ya juhudi za VETA katika kujenga Taifa lenye wananchi wenye ujuzi watakaoweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.