Serikali inaendelea kuhakikisha maeneo ya kazi kwa watumishi wa umma ni salama ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya kiwango.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) katika kikao na watumishi wa Wizara ya Maji, Mtumba jijini Dodoma leo amesema Serikali itasimamia maslahi bora kwa watumishi na sio maneno.
“Tufanye kazi vizuri na kwa ubora, mimi nitawapigania katika kazi ili Sekta ya Maji itimize lengo la Serikali” Waziri Aweso amesema na kusisitiza ni vizuri kila mtumishi kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo mbalimbali ya serikali.
Waziri Aweso amesema na kuwataka watumishi kujivunia kazi kubwa wanayofanya na wawe walimu popote watakapokuwa kuhusu utekelezaji wa kazi na kufikisha huduma ya maji katika jamii.
Amesisitiza watumishi kukumbuka familia pamoja na majukumu wanayotekeleza kwa kusisitiza “Mwenda kwao haogopi giza” kwa sababu kuijali familia ni baraka ya Mwenyezi Mungu ambayo ataweka wepesi katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Waziri Aweso amewakumbusha watumishi wote kuishirikisha jamii katika kazi ili kuwa na uelewa wa pamoja na manufaa ya kazi kujulikana mapema katika jamii.
Mhe. Aweso ameainisha vipaumbele nane kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kuwa ni pamoja na kukamilisha uandaaji wa Mpango mkuu wa rasilimali za maji nchini, ukamilishaji wa mchakato wa matumizi ya Dira janja, utafutaji wa vyanzo mbadala vya Fedha, utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji, uanzishwaji wa makavazi ya wizara, mpango wa kufikisha maji ya ziwa Victoria Dodoma na kuwa na Ramani mahsusi ya mtandao wa mfumo wa maji kwa Sekta ya Maji nchi nzima.
“Ili kutimiza malengo haya lazima tuhakikishe sisi kama viongozi tunawatengenezea watumishi wetu mazingira mazuri ya kazi na ile dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani inatimia” Aweso amesema.
Pamoja na hayo amewataka wataalamu kuhakikisha mifumo yote ya Taasisi za wizara inasomana na wizara ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi.

