Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi wamehimiza kuharakishwa kwa utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), ili kuhakikisha uwekezaji unaofanywa katika bonde hilo unaleta tija na manufaa kwa wananchi.

Msisitizo huo umetolewa katika kikao kilichofanyika Septemba 3, 2026 jijini Dodoma, kufuatia ziara iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Bw. Charles Ngeleja Kadonya, ya kutembelea na kukagua programu na miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria katika Kanda ya Ziwa.

Miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele ni kuanza kutoa huduma kwa Kituo cha Kikanda cha Uratibu wa Utafutaji na Uokoaji katika Ziwa Victoria (MRCC), ambacho hakijaanza kutoa huduma kutokana na changamoto za watumishi na taratibu za kugharamia uendeshaji wake.

Kikao kimearifiwa kuwa ridhaa ya kupeleka watumishi waliopendekezwa katika kituo hicho tayari imetolewa. Aidha, imekubaliwa kuboresha Mkataba wa Ufadhili kati ya Tanzania na Uganda ili kuwezesha Tanzania kugharamia moja kwa moja uendeshaji wa muda wa kituo hicho katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Kikao pia kimeweka msisitizo katika kupanua matumizi ya Meli ya MV New Mwanza ili iweze kufanya safari katika nchi jirani, hususan Uganda. Wataalamu kutoka TASHICO, TRC na TPA tayari wamefanya tathmini ya miundombinu ya Bandari ya Port Bell nchini Uganda na kuandaa mapendekezo yatakayowezesha meli hiyo kuanza safari nchini humo.

TASHICO imeelekezwa kuwasilisha mapendekezo hayo kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa hatua zaidi. Vilevile, Wizara ya Uchukuzi imeshauriwa kuangalia upya mfumo wa tozo za meli katika Bandari za Mwanza ili kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza ushindani.

Katika hatua nyingine, Tume ya Taifa ya Mipango imeahidi kufanyia kazi Andiko la Programu Mtambuka ya Kutatua Changamoto za Maendeleo katika Ziwa Victoria na kutoa ridhaa ya kuendelea na hatua inayofuata ndani ya siku 14.

Kwa upande wa Mradi wa Upanuzi wa Mtandao wa Majitaka na Usafi wa Mazingira Mwanza, MWAUWASA imepata ridhaa kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kuendelea na hatua inayofuata na sasa inaandaa taratibu za kumpata mkandarasi.

Aidha, Wizara ya Maji imeahidi kufanyia kazi changamoto ya miundombinu ya maji katika Mradi wa Majaribio wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika Kijiji cha Ng’haya, Magu, kwa kushirikiana na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria.

Kikao kimehitimishwa kwa kuzitaka Wizara na Taasisi husika kuendelea kushirikiana katika kutekeleza maazimio na makubaliano yaliyofikiwa, ili kuhakikisha miradi na programu hizo zinatekelezwa kwa ufanisi, kwa wakati na kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.