……………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Profesa Preksedis Ndomba akiambatana na Mkurugenzi wa Kampasi ya DIT Mwanza, Dk Albart Mmari, na Mkuu wa Idara ya Mafunzo Viwandani Dk John Msumba wametembelea Kampuni ya kutengeneza viatu ya BORA ikiwa ni hatua za awali katika kuingia ushirikiano.
Timu hiyo kutoka DIT imepata nafasi ya kutembelea kiwanda hicho cha BORA kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na kiwanda hicho.
DIT ambayo Kampasi ya Mwanza inatoa mafunzo ya uchakataji ngozi ikiwa ni pamoja na utengenezaji viatu, itanufaika kwa Wakufunzi wake kuongeza ujuzi na utaalamu kiwandani halo na pia wanafunzi watapata nafasi ya kujifunza kwa vitendo katika kiwanda hicho na kwa upande wa kiwanda watanufaika kwa kupata wataalamu kutoka DIT.
Kwa mujibu wa Profesa Ndomba, DIT kupitia kampasi ya Mwanza inalenga kuwa kituo cha umahiri katika utengenezaji wa bidhaa za ngozi na teknolojia zake ambapo Mkurugenzi Mkuu wa BORA, Rajesh Sajinan aliahidi kushirikiana na DIT ili kupata wataalamu.
Makubaliano ya ushirikiano baina ya Taasisi hizo yatatiwa saini siku za karibuni baada ya kukamilika kwa taratibu muhimu za kiutendaji.