Dar es Salaam, Septemba 3, 2026
Wananchi wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kupigia kura kazi 294 za uandishi wa habari na makala za maendeleo zilizofuzu katika Samia Kalamu Awards 2026.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 3, 2026, na Mwakilishi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa habari (JAB) Prudence Constantine, wakati wa mkutano wa kutangaza kuanza kwa zoezi la upigaji kura litakalodumu hadi Septemba 30, 2026.
Prudence amesema kura za wananchi ni sehemu muhimu ya mchakato wa kumpata mshindi, kwa kuwa zinatoa nafasi kwa jamii kutambua na kuunga mkono kazi zilizoleta mchango au athari chanya katika maisha ya watu na maendeleo ya Taifa.
Amesema wananchi, wakiwa watumiaji wa maudhui ya habari, wana nafasi ya kuchagua kazi wanazoona zimefanya vizuri, zimeakisi mahitaji na maslahi ya jamii na kusaidia kuibua au kuelimisha kuhusu masuala muhimu ya maendeleo.
Wananchi wanaweza kupiga kura kupitia tovuti ya www.samiaawards.tz na kufuata maelekezo yaliyowekwa ili kuchagua kazi wanayoipendelea.
Pia, kura zinaweza kupigwa kupitia ujumbe mfupi wa maandishi kwa kutuma neno “SKA”, likifuatiwa na namba ya mshiriki kwenda 15200.
Akizungumza kuhusu Kazi 294 zilizofuzu kupigiwa kura Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandishi Peter Mwasalyanda amesema kazi hizo zimefuzu baada ya tathmini ya kazi 3,003 zilizowasilishwa na waombaji 985. Jopo la majaji lilifanya tathmini kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na kuteua kazi zilizopata alama za juu.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt, Rose Reuben amewapongeza waandishi wa habari walioshiriki kuwasilisha makala zao katika shindano la Samia Kamalu Awards 2026 ambapo sasa baadhi zimechaguliwa kuingia awamu ya kupigiwa kura na wananchi zoezi ambalo linaanza leo Septemba 3, 2026.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt, Rose Reuben amewakaribisha wananchi kushiriki katika zoezi la kupiga kura kwa kuwa wananchi ndio walaji wa habari na kutambua maudhuri ambayo yamewaguswa katika maeneo yao na kuamua kama zinaweza kushinda.
“Kura ya wananchi ni ya muhimu sana kwa sasa kwa kuendeleza na kutambua maudhui ya ndani, kwa kuitangaza nchi kutambulika kimataifa kupitia habari zilizondikwa kwa weledi na waandishi wa habari mahiri walioshiriki katika shindano la SKA 2026”. Dkt Rose Reuben – Mkurugenzi Mtendaji TAMWA
“Kwa tathmini yetu ya majaji wa SKA 2026 wakati tunapitia makala zilizowasilishwa tumebaini kuwa waandishi wa habari wa Tanzania wanauwezo mkubwa wa kuibua masuala mbalimbali ya maendeleo katika ngazi zote nchini”. Mmoja wa majaji SKA 2026 Bi, Beatrice Bandawe
Samia Kalamu Awards zinaandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA kwa Kuhsirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) pamoja na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) zikilenga kutambua, kuenzi na kuhamasisha ubora, weledi na ubunifu katika uandishi wa habari na utayarishaji wa makala za maendeleo nchini.

