
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) imesisitiza kasi, ubora na ujenzi unaokwenda sambamba na mahitaji ya soko, ikieleza kuwa NHC ya sasa lazima iwe na uwezo wa kushindana kwa ubora na wawekezaji binafsi katika sekta ya nyumba.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Bodi ya NHC, Dkt. Sophia Kongela, baada ya Bodi kufanya ziara ya kukagua miradi ya Samia Housing Scheme Medeli, Njedengwa Valley View na Iyumbu Urban Apartments jijini Dodoma.
Ziara hiyo iliyohusisha wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya NHC imelenga kujionea hatua za utekelezaji wa miradi, ubora wa kazi na namna Shirika linavyotekeleza dhamira yake ya kuongeza nyumba za kisasa katika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Kongela amesema Bodi imeridhishwa na mabadiliko yanayoonekana katika utekelezaji wa miradi na juhudi kubwa zinazofanywa na wahandisi pamoja na Menejimenti ya Shirika.
«“Ukipita kwenye miradi yetu sasa unaona kabisa nguvu kubwa iliyowekwa na kazi inayofanywa na wahandisi wetu. Tunachotaka sasa ni kuona kasi hii inaendelea na ile habari ya kuchelewa kuingiza nyumba zetu sokoni isiwepo tena,” amesema Dkt. Kongela.»
Amesisitiza kuwa kasi pekee haitoshi, bali nyumba zinazojengwa na NHC lazima ziwe na ubora, usanifu wa kisasa na thamani inayolingana na matarajio ya wateja.
«“Watu wa sasa wanataka vitu vizuri. Ukilinganisha nyumba zetu na za private developer mwingine, NHC lazima iwe kwenye viwango vya juu. Tunataka kutoa bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na kuzifikisha sokoni kwa wakati,” amesema.»
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, amesema Menejimenti imejipanga kutekeleza maelekezo ya Bodi, huku hatua mbalimbali zikiwa zimechukuliwa kuondoa sababu zilizokuwa zikichelewesha miradi hapo awali.
Amesema Shirika sasa lina mikataba ya muda mrefu na wasambazaji wa vifaa vya ujenzi, hatua inayosaidia kuhakikisha maeneo ya miradi yanapata vifaa kwa wakati bila kusimamisha kazi.
«“Katika sites zetu hakuna uhaba wa building materials. Timu zetu pia zinafanya kazi kwa kujituma sana; pale inapohitajika kazi zinaendelea hata nje ya muda wa kawaida ili kuhakikisha ratiba zetu hazirudi nyuma,” amesema Abdallah.»
Ameongeza kuwa katika baadhi ya miradi, utekelezaji uko mbele ya ratiba kwa takribani mwezi mmoja, huku NHC ikiendelea kuwekeza katika vifaa na teknolojia za kisasa za ujenzi ili kuongeza kasi na kuhakikisha ubora.
Ziara hiyo ya Bodi jijini Dodoma imeonesha picha moja kubwa—NHC inataka kwenda mbele, si kurudi nyuma; kujenga kwa kasi, kwa ubora na kupeleka sokoni nyumba zinazoweza kushindana katika soko la kisasa la makazi.
Kwa NHC, sasa si suala la kujenga nyumba pekee; ni kujenga kwa kiwango, kukamilisha kwa wakati na kumpa mteja thamani ya fedha yake.
