
Ofisa Masoko wa Kijani Consultant, Franswer Lawrence, leo akitoa elimu kwa wananchi kwenye Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF 2026), yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha, Wilaya ya Ilemela, Mwanza.Picha zote na Baltazar Mashaka
…….
Na BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
WAKULIMA wa mahindi na mpunga wametakiwa kutumia mbegu bora zilizoboreshwa zinazostahimili ukame, magonjwa na wadudu waharibifu ili kuongeza tija na mavuno katika kilimo, hasa wakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ushauri huo umetolewa leo na Ofisa Masoko wa Kijani Consultant, Franswer Lawrence, wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF 2026), yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha, Wilaya ya Ilemela, Mwanza.
Lawrence alisema uchaguzi wa mbegu bora kulingana na mazingira ya eneo la mkulima ni hatua muhimu ya kuongeza uzalishaji, kwani baadhi ya mbegu zimeboreshwa kuwa na uwezo wa kustahimili ukame na changamoto nyingine zinazoweza kupunguza mavuno.
Alisema miongoni mwa mbegu za mahindi zinazopendekezwa ni SITUKA M1, ambayo ina uwezo wa kuvumilia ukame na magonjwa.
Kwa mujibu wa Lawrence, SITUKA M1 inapendekezwa kupandwa katika maeneo yenye mwinuko wa mita 1,000 hadi 1,500 kutoka usawa wa bahari na hukomaa ndani ya siku 110 hadi 120.
Alisema mbegu hiyo ina uwezo wa kubeba mahindi mawili kwa shina moja na inashauriwa kupandwa kwa nafasi ya sentimita 75 kwa 30.
“Mbegu hii ina uwezo wa kuvumilia ukame na magonjwa, inakomaa ndani ya siku 110 hadi 120 na inaweza kubeba mahindi mawili kwa shina moja. Inashauriwa ipandwe kwa nafasi ya sentimita 75 kwa 30,” alisema.
Akizungumzia mbegu nyingine ya mahindi, Lawrence alisema T105 pia imeboreshwa kuwa na uwezo wa kuvumilia ukame, magonjwa na wadudu waharibifu.
Alisema T105 inapendekezwa kupandwa katika maeneo yenye mwinuko wa mita 800 hadi 1,500 kutoka usawa wa bahari na hukomaa ndani ya siku 105 hadi 115.
Alisema mbegu hiyo pia ina uwezo wa kubeba mahindi mawili kwa shina moja na wakulima wanapaswa kuzingatia nafasi inayopendekezwa wakati wa kupanda ili kupata matokeo mazuri.
Kwa upande wa zao la mpunga, Lawrance alisema SARO 5 (TDX 306) inafaa kwa kilimo cha mabondeni, mbugani na maeneo yenye mifumo ya umwagiliaji.
Alisema kwa ekari moja, mkulima anayepandikiza anahitaji takribani kilo 15 za mbegu, wakati anayemwaga mbegu anahitaji kilo 30.
“Kwa mpunga aina ya SARO 5, mkulima anaweza kupata mavuno kati ya gunia 25 hadi 50 kwa ekari, kutegemea matumizi ya kanuni bora za kilimo,” alisema.
Alisema mbegu hiyo ina uwezo wa kuvumilia magonjwa ya mpunga, ikiwamo madoadoa ya njano, huku mchele unaozalishwa ukiwa na harufu nzuri na ladha inayopendwa na walaji.
Kwa mujibu wa Lawrence, mmea wa mpunga aina hiyo hukua hadi kufikia urefu wa takribani mita moja na mchele wake una sifa ya kuwa mtamu.
Aliwataka wakulima kutofanya uchaguzi wa mbegu kwa kuangalia jina au bei pekee, bali kuzingatia mazingira ya kilimo, aina ya udongo, upatikanaji wa maji na ushauri wa wataalamu ili kupata matokeo yanayotarajiwa.
Lawrence pia aliwataka wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo baada ya kuchagua mbegu, ikiwamo maandalizi sahihi ya mashamba, matumizi sahihi ya mbolea, udhibiti wa magonjwa na wadudu waharibifu pamoja na kuvuna kwa wakati.
Alisema elimu inayotolewa katika maonesho hayo inalenga kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwasaidia kupata taarifa sahihi kuhusu mbegu na teknolojia za kilimo zinazoweza kuongeza tija na kipato.
“Tunataka mkulima apate elimu sahihi kabla ya kuchagua mbegu, kwa sababu mazingira ya kilimo hutofautiana. Mbegu inayofaa eneo moja si lazima ifanye vizuri katika eneo jingine,” alisema.
Alisema matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame ni muhimu kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoathiri mifumo ya mvua na kuongeza hatari ya wakulima kupata mavuno hafifu.
Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF 2026) yanafanyika katika Uwanja wa Furahisha, Ilemela, Mwanza, yakiwa na kaulimbiu “ Amani na Usalama ni Kichocheo cha Biashara na Uwekezaji,” yakishirikisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi.
