Mhitimu wa Chuo cha IFM Kampasi ya Mwanza,  Gladness Michael Silayo (kushoto), akiwaonesha wateja viatu vinavyotengenezwa katka kiwanda chake cha Pacha Shoes Company, leo kwenye maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki, Uwanja wa Furahisha, Ilemela.

………..

Na BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

MHITIMU wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Gladness Michael Silayo, amegeuza elimu ya Shahada ya Uhasibu na Fedha kuwa fursa ya ujasiriamali kwa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza viatu cha Pacha Shoes Company, kwa kutumia ngozi inayopatikana nchini.

Silayo, aliyehitimu mwaka 2023, alianza biashara hiyo mwaka 2023 ambapo wazo la kuanzisha kiwanda, alilipata Septemba , mwaka 2023, alipokwenda kufunga ndoa na mumewe, ili kukabiliana na changamoto ya kupata ajira, na kwa sasa ameajiri wafanyakazi kadhaa.

Bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho zimekuwa kivutio kikubwa katika Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF 2026), yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha, Wilaya ya Ilemela, Mwanza, huku wananchi wakifurika katika banda la IFM kutazama na kujua zaidi kuhusu viatu hivyo vinavyotengenezwa kwa kutumia ngozi ya ndani.

Akizungumza jana wakati wa maonesho hayo, Silayo alisema baada ya kushindwa kupata ajira aliamua kutumia maarifa aliyoyapata chuoni kuanzisha biashara ya uzalishaji wa viatu, akiamini kuwa ujasiriamali ungekuwa njia ya kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine.

“Elimu ya ujasiriamali niliyopata imenisaidia. Namshukuru sana Dkt. Laurent Sunda, alikuwa akitufundisha somo la ujasiriamali na kutushauri vijana kuwa wabunifu,” alisema na kuongeza kuwa,  akiwa chuoni pia alianza kutengeneza bidhaa ya mafuta ya kupaka, hatua iliyomsaidia kujenga ujuzi wa vitendo na kumwandaa kwa shughuli za uzalishaji baada ya kuhitimu.

Silayo alisema wazo la kuanzisha uzalishaji wa viatu lilitokana na utafiti alioufanya kuhusu mahitaji ya soko, ambapo alibaini kuwa kuna mahitaji ya viatu vyenye ukubwa maalumu na ubora unaodumu.

“Kwa kweli niliona viatu ni fursa kibiashara maana kila mtu anahitaji kuvaa viatu. Mwanza niliona viatu vinavyotengenezwa havina ubora wa kudumu kwa miaka miwili, nilianza kutengeneza vya wanafunzi,” alisema.

Msomi huyo wa Shahada ya Uhasibu na Fedha alisema tangu aanze uzalishaji amekuwa akifanya utafiti na kuboresha bidhaa zake, ikiwamo kutafuta malighafi na teknolojia zinazoweza kuongeza uimara wa viatu hivyo.

“Nimeboresha bidhaa yangu, natumia gundi ya moto ambayo ni gharama kubwa, tunaichanganya na gundi aina nyingine, inasababisha viatu visibanduke,” alisema.

Hata hivyo, alisema pamoja na mwitikio mzuri wa wananchi kwa bidhaa hizo, changamoto kubwa inayomkabili ni upatikanaji wa soko kutokana na gharama za uzalishaji kuwa kubwa ikilinganishwa na bidhaa nyingine zinazouzwa kwa bei ya chini.

Alisema hali hiyo inafanya baadhi ya wateja kuangalia zaidi bei kuliko ubora wa bidhaa, jambo linaloweka changamoto kwa wazalishaji wanaotumia malighafi bora za ndani na kuzingatia ubora katika uzalishaji.

“Changamoto kubwa ni soko. Gharama za uzalishaji ni kubwa, hivyo bidhaa zetu zinakuwa na bei ambayo wakati mwingine ni kubwa ikilinganishwa na viatu vya bei ya chini vilivyopo sokoni. Tunahitaji kupata masoko zaidi ili uzalishaji uweze kuendelea na biashara ikue,” alisema.

Silayo alisema maonesho ya MEATF 2026 yamempa fursa ya kuitangaza biashara yake kwa wananchi na wadau mbalimbali, kupata maoni kuhusu bidhaa hizo na kutafuta fursa zaidi za masoko ambapo mwitikio wa wananchi katika banda hilo umempa hamasa ya kuendelea kuboresha bidhaa na kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Utawala wa IFM, Kampasi ya Mwanza, Dkt. Laurent Joseph, akizungumzia ubunifu uliofanywa na mhitimu wa chuo hicho kwa kutumia malighafi za ndani, alisema  ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuchangia katika kutatua changamoto ya ajira na kukuza uchumi.

Dkt. Joseph alisema matumizi ya malighafi za ndani yanaweza kupunguza utegemezi wa malighafi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, huku yakitoa nafasi kwa Watanzania kuongeza thamani ya rasilimali zinazopatikana nchini.

Naye Mhadhiri Msaidizi na Mkuu wa Taaluma wa IFM, Kampasi ya Mwanza, Bahati Maneno, alisema ushiriki wa chuo hicho katika MEATF 2026 umefungua fursa ya jamii kufahamu shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo, ikiwamo tafiti, ushauri wa kitaalamu na kuwaandaa vijana wenye uwezo wa kujiajiri.

“Mafanikio ya wahitimu kama Silayo yanaonesha umuhimu wa elimu ya juu katika kuwawezesha vijana kutumia maarifa yao kuanzisha shughuli za uzalishaji na kutoa ajira kwa wengine.Kwa sasa, banda la IFM limeendelea kuwa kivutio kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo,” alisema.

Maneno alisema bidhaa za ubunifu zinazotumia malighafi za ndani, zikiwamo viatu vya ngozi vya Silayo, zinatumika kuonesha uwezo wa vijana katika kuongeza thamani ya malighafi na kuzalisha bidhaa zinazoweza kushindana sokoni.

Maonesho ya MEATF 2026 yanafanyika yakiwa na kaulimbiu: ‘Usalama na Amani ni Kichocheo cha Biashara na Uwekezaji,’ ikiwakutanisha wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji kutoka sekta ya umma na binafsi.