Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda akiongea na Menejimenti ya NCAA wakati wa uzinduzi wa mfumo wa Utalii kwa Njia ya Mtandao (Tourism Web Camera) katika Ofisi za Mamlaka hiyo.
Sehemu ya wajumbe wa Menejimenti ya NCAA wakifuatilia uzinduzi huo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda (wa pili kulia) akizungumza na Kamishna wa Uhifadhi NCAA Dkt Freddy Manongi (kushoto) na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo (Kulia) baada ya uzinduzi wa mfumo wa Utalii kwa nia ya Mtandao.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Freddy Manongi akimueleza katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii (hayuko pichani) jinsi mfumo wa Utalii Mtandao utakavyowezesha wadau mbalimbali kuona vivutio vya Ngorongoro popote Duniani.
…………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu-NCAA
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imezindua mfumo mpya wa Utalii Mtandao “Tourism Web Camera” unaolenga kuwaleta pamoja watu mbalimbaali duniani kuona vivutio vilivyopo katika hifadhi ya Ngorongoro hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 ambapo wageni wengi wamefungiwa katika nchi zao.
Uzinduzi wa Mfumo huo uliohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda umelenga kuunganisha watu mbalimbali ulimwenguni kuweza kufuatilia vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo ambapo kwa kuanzia watazamaji wataona vivutio hivyo bure na baadae kuchangia kiasi kidogo cha pesa katika kuendeleza uhifadhi wa rasilimali na vivutio katika hifadhi hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda ameelezea kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na NCAA katika kuwafikia wadau wake pamoja na kukabiliana na changamoto za ukosefu wa wageni kutokana na Janga la Korona.
Amebainisha kuwa shughuli za ulinzi na uhifadhi wa rasilimali ndani ya hifadhi ni suala endelevu na lazima kuendelea kuwahabarisha wageni kuhusu yanayojiri ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro hasa kipindi hiki ambacho wengi wamezuliwa kusafiri.
“Tunajua kuwa kwa sasa watalii wengi nchi zao ziko kwenye ‘lockdown’ na hawawezi kusafiri, NCAA mmefanya kitu chenye maana katika kutafuta namna ya kuwafikia hukohuko walipo na kuendelea kufurahia utalii wa Ngorongoro popote duniani, ni imani yangu kuwa hatua hii itasaidia kuwaandaa watu kisaikolojia wasisahau kuhusu vivutio vya Ngorongoro hata baada ya janga hili kupita” ameongeza Prof Mkenda.
Prof Mkenda ameongeza kuwa Mtazamo wa Rais Dkt John Pombe Magufuli ni kuhakikisha kuwa tunaendelea kujilinda na kujipanga huku tukihakikisha kuwa baada ya janga la CORONA kupita uchumi wa nchi yetu unarudi kama ulivyokuwa.
Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt Freddy Manongi amebainisha kuwa mfumo huo wa utalii mtandao kwa njia ya “Live streaming web camera” uliozinduliwa unalenga kuwafikia watu mbalimbali duniani kuona bure kwa kufungua Youtube channel na kuandika neno Ngororongoro Conservation Areakwa ajili ya kufuatilia vivutio katika hifadhi hiyo.
“Tumeshuhudia anguko katika sekta ya Utalii baada ya janga la Covid 19 ambapo kwa sasa inapita siku nzima bila kupata mgeni hata mmoja, kwa hiyo tumeamua kubuni teknolojia hii ya kuwaleta pamoja wateja wetu duniani kote ambao kupitia mfumo huu wataona vivutio vya Ngorongoro Mubashara wakiwa majumbani mwao”
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa NCAA anayesimamia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Bw. Jocktan Bikombo amebainisha kuwa mfumo huo wa ‘live streaming’ umeunganishwa na Camera mbalimbali zilizofungwa ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ili kuhakikisha kuwa wateja wetu wanapata ladha tofauti ya vivutio vilivyopo.
Uzinduzi wa mfumo huo umeenda sambamba na majaribio ya kuunganisha moja kwa moja wadau mbalimbali waliopo Paris nchini Ufaransa na London Nchini Uingereza ambao wamethitbitisha kuuona na kushuhudia vivutio hivyo kwa njia ya mtandao.