NA DENIS MLOWE, IRINGA 
TAMASHA Kubwa la watumishi kutoka taasisi mbalimbali za serikali linatarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii katika viwanja vya Mkwawa mkoani Iringa, likiwa na lengo la kuwaunganisha watumishi na kujenga mahusiano mazuri nje ya maeneo yao ya kazi.
Tamasha hilo linaloandaliwa na taasisi ya Iringa Finest, litahusisha michezo na burudani mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba, kukimbia kwenye magunia, mbio za vijiti, kurusha pete, kufukuza kuku, kula mashindano, mashindano ya kubeba vitu, pamoja na michezo mingine ya kijamii itakayowapa washiriki nafasi ya kujiburudisha na kushirikiana.
Mratibu wa tamasha hilo, Pastory Kwambiana, akizungumza na Full Shangwe amesema maandalizi ya tamasha hilo yamefikia asilimia 80 na kwamba wanatarajia kushirikisha taasisi mbalimbali za serikali.
Amesema tamasha hilo limeandaliwa kwa lengo la kuwapatia watumishi nafasi ya kukutana, kufahamiana na kujenga mshikamano, kutokana na ukweli kwamba baadhi yao hawapati nafasi ya kukutana mara kwa mara kutokana na majukumu yao ya kila siku.
“Lengo kubwa ni kuwakutanisha watumishi ambao hawakutani mara kwa mara, ili wapate nafasi ya kufahamiana, kushirikiana na kuwa kitu kimoja kupitia michezo na burudani,” amesema Kuambiana.
Amesema maandalizi yanaendelea kwa kasi ili kuhakikisha shughuli zote zinakwenda vizuri siku ya tamasha, huku akiwataka watumishi na taasisi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hilo.
Tamasha hilo linatarajiwa kuwa sehemu ya burudani na kujenga mahusiano baina ya watumishi, huku michezo mbalimbali ikitarajiwa kuongeza hamasa na ushindani miongoni mwa washiriki.