Katibu wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiraia Mkoa wa Arusha, Elisante Ephrhim akizungumza kwenye jukwaa hilo jijini Arusha
Na Happy Lazaro, Arusha.
Katibu wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiraia Mkoa wa Arusha, Elisante Ephrhim amesema mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanapaswa kuongeza ubunifu na kutumia rasilimali zilizopo ndani ya jamii ili kujenga uendelevu wa taasisi hizo na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka nje ya nchi.
Akizungumza katika Jukwaa la Maendeleo la Wadau lililofanyika mkoani Arusha, amesema zaidi ya wadau 500 kutoka mashirika yanayotekeleza shughuli katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Arusha walishiriki katika jukwaa hilo kwa lengo la kujadili ripoti, ubia, fursa na namna ya kuimarisha maendeleo ya mashirika.
Amesema kaulimbiu ya jukwaa hilo imejikita katika ubunifu, ubia na uendelevu wa mashirika kupitia rasilimali za ndani, akieleza kuwa ni muhimu kwa NGOs kukaa pamoja na kutambua fursa zilizopo katika mkoa huo na kuzitumia kama chanzo cha kujiendesha na kuendeleza shughuli zao.
“Tumekaa pamoja kuangalia ni fursa zipi zilizopo hapa Arusha ambazo zinaweza kutusaidia kupata rasilimali za kuendesha mashirika yetu, badala ya kutegemea zaidi fedha kutoka kwa wafadhili wa nje,” amesema
Amesema kupungua kwa fedha kutoka kwa wafadhili wa nje kunapaswa kuwa changamoto inayowasukuma viongozi wa NGOs kubuni vyanzo vipya vya mapato, kuimarisha ushirikiano na kutumia fursa zilizopo katika jamii badala ya kusubiri misaada kutoka nje.
Aidha, amewataka vijana kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana kutokana na shughuli kubwa za kimataifa zinazofanyika nchini, ikiwemo fursa katika biashara, malazi, huduma za usafiri, utalii, ukarimu na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wageni.
Ameongeza kuwa , vijana wanapaswa kuwekeza nguvu, maarifa na ubunifu katika kuzitumia fursa hizo, akisisitiza kuwa mafanikio hayaji kwa urahisi bali yanahitaji juhudi, maarifa na utayari wa kujifunza na kufanya kazi.
Ametumia mfano wa mmea unaochipua na baadaye kukua kuwa mti mkubwa, akisisitiza kuwa ni wakati kwa vijana kuchukua hatua na kutumia fursa zilizopo sasa ili kujenga msingi imara wa maisha yao, jamii zao na taifa kwa ujumla.
“Fursa hizi si rahisi, zinahitaji nguvu, akili na maarifa. Vijana tutumie nguvu na uwezo tulionao, tufanye ubunifu, tutafute fedha na rasilimali ili tujenge jamii bora ambayo wazee wetu na taifa kwa ujumla watajivunia,” amesema.
