Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimekubaliana kuondoa jambo la 15 la Maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na gesi asilia katika orodha ya mambo ya Muungano.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambwe Mhe. Rashid Habib Ali Rashid aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuondoa suala la Mafuta na Gesi kwenye orodha ya Masuala ya Muungano.

Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Kwagilwa alisema kwa sasa, suala la Mafuta na Gesi Asilia linasimamiwa na kila upande ambapo SJMT imetunga Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia ya Mwaka 2015 ambayo chini ya kifungu cha 11 imeanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA – Petroleum Upstream Regulatory Authority).

Aliongeza kuwa kwa upande wa Zanzibar, SMZ imetunga Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia, Namba 6 ya Mwaka 2016 iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti, Utafutaji na Uendelezaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA Zanzibar Petroleum Regulatory Authority) na Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC Zanzibar Petroleum Development Corporation).

Mheshimiwa Naibu Spika Kwanza niungane na Mheshimiwa mbunge ambaye amesema kwamba Baraza la Wawakilishi lilisharidhia na lilishawasilisha kutaka suala hili liondolewe na ndio maana Baraza la Wawakilishi limetunga sheria ya kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti na hivyo linashughulikiwa katika kila upande hivyo halina hoja kinzani, alifafanua Kwagilwa.

Pamoja na hayo, kila ongezeko au kuondolewa kwa masuala ya Muungano hupata nafasi ya kujadiliwa na kupata ridhaa ya Serikali zote mbili ya SJMT na SMZ na kupitia mchakato mahususi wa kikatiba.

Mabadiliko husika hupitia katika Baraza la Wawakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara ya 98(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaruhusu Bunge kutunga sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini kwa utaratibu maalumu ufuatao ulioainishwa na Katiba.