Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), kwa kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA), imeanza kuimarisha maandalizi ya usalama wa nyuklia na mionzi kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji kwa pamoja na Kenya na Uganda.
Maandalizi hayo yanalenga kujenga uwezo wa kitaifa wa kuzuia, kubaini na kukabiliana na vitisho vinavyoweza kuhusisha nyenzo za nyuklia au vyanzo vingine vya mionzi wakati wa mashindano hayo, ambayo yanatarajiwa kuvutia wachezaji, viongozi, mashabiki, waandishi wa habari na wageni kutoka mataifa mbalimbali.
Akifungua rasmi jijini Arusha warsha ya siku tano kuhusu uandaaji na utekelezaji wa hatua za usalama wa nyuklia katika matukio makubwa ya umma, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Najat Kassim Mohammed, amesema ukubwa na hadhi ya AFCON 2027 vinahitaji maandalizi ya kina na ushirikiano wa taasisi mbalimbali ili kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika katika mazingira salama.
Warsha hiyo, inayofanyika kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 4, 2026, inawakutanisha wataalamu na maofisa kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi Tanzania, vyombo vya usalama, mamlaka zinazohusika na forodha na uhamiaji, wasimamizi wa viwanja vya michezo pamoja na taasisi nyingine zenye majukumu katika ulinzi na usalama.
Profesa Najat amesema maandalizi ya mashindano yenye hadhi ya AFCON hayaishii katika ujenzi na uboreshaji wa viwanja na miundombinu mingine pekee, bali yanapaswa kwenda sambamba na kuimarisha mifumo ya usalama kwa ajili ya kulinda wananchi na wageni watakaokuwa nchini wakati wa mashindano hayo.
Amesema mikusanyiko mikubwa ya kimataifa inahitaji maandalizi yanayozingatia aina mbalimbali za vitisho na hatari zinazoweza kujitokeza, hivyo ni muhimu kwa taasisi zinazohusika kuwa na uwezo wa kubaini mapema jambo lolote lisilo la kawaida na kuchukua hatua stahiki kwa wakati.
“Ni lazima kuhakikisha kuwa vifaa vya mionzi na nyenzo nyingine zinazohusiana na nyuklia hazitumiki kwa madhumuni ya uhalifu, uharibifu au matumizi mengine yasiyoruhusiwa wakati wa AFCON 2027,” amesema Profesa Najat.
Amesisitiza kuwa usalama wa nyuklia katika matukio makubwa ya umma hauwezi kusimamiwa na taasisi moja pekee, bali unahitaji ushirikiano wa karibu, uratibu na ubadilishanaji wa taarifa kati ya taasisi zote zenye wajibu katika mfumo wa kitaifa wa ulinzi na usalama.
Kwa mujibu wa Profesa Najat, mafanikio katika eneo hilo yatategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa taasisi zinazohusika kufanya kazi kwa pamoja, kila moja ikifahamu wajibu wake na namna ya kushirikiana na taasisi nyingine kabla, wakati na baada ya tukio.
Amesema warsha hiyo ni sehemu ya maandalizi yanayolenga kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa taasisi zinazohusika, kuimarisha uwezo wa wataalamu na kuhakikisha mifumo ya uratibu inafanya kazi kwa ufanisi endapo kutatokea tukio linalohitaji hatua za kiusalama.
Tanzania tayari imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha uwezo wake katika eneo la usalama wa nyuklia na mionzi, ikiwemo matumizi ya vifaa vya kugundua mionzi katika baadhi ya maeneo muhimu na mipakani, pamoja na kuwajengea uwezo maofisa walio mstari wa mbele katika kubaini na kukabiliana na matukio yanayoweza kuhusisha vyanzo vya mionzi.
Profesa Najat amesema pamoja na uwepo wa vifaa hivyo, jambo la msingi ni kuhakikisha wataalamu wana uwezo wa kuvitumia kwa usahihi na taasisi zinazohusika zinafahamu hatua zinazopaswa kuchukuliwa baada ya kubainika kwa tukio linalohitaji uchunguzi zaidi.
Katika kipindi cha siku tano, washiriki watapatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo kuhusu hatua za kuzuia vitisho kabla ya tukio, namna ya kuendesha operesheni za usalama katika matukio makubwa, utambuzi wa mionzi, tathmini ya tahadhari, taratibu za upekuzi na matumizi ya vifaa mbalimbali vya kugundua mionzi.
Miongoni mwa vifaa vitakavyotumika katika mafunzo hayo ni Personal Radiation Detectors (PRDs), Radioisotope Identification Devices (RIDs) pamoja na vifaa vya kugundua mionzi vinavyobebwa mgongoni. Washiriki watafundishwa namna ya kutumia vifaa hivyo, kutambua tahadhari zinazotolewa na kufanya tathmini kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.
Mafunzo pia yatahusisha taratibu za kufanya uchunguzi kwa watu na magari, namna ya kuthibitisha tahadhari inayotolewa na vifaa vya kugundua mionzi, pamoja na taratibu za kushughulikia vifurushi vinavyotiliwa shaka.
Profesa Najat amesema sehemu muhimu ya warsha hiyo itakuwa mazoezi ya vitendo yatakayowawezesha washiriki kutumia maarifa watakayopata darasani katika mazingira yanayofanana na hali halisi ya tukio kubwa la umma.
Washiriki watagawa majukumu katika timu mbalimbali, zikiwemo timu ya uongozi wa operesheni, timu za utafutaji na timu ya msaada wa kitaalamu wa masuala ya mionzi. Timu hizo zitafanya maandalizi ya uchunguzi wa eneo kabla ya tukio, kuandaa namna ya kukabiliana na hali mbalimbali na kugawana majukumu kulingana na wajibu wa kila upande.
Mazoezi hayo yatahusisha pia uchunguzi wa kimionzi katika mazingira ya uwanja wa michezo, ikiwemo eneo la uwanja na sehemu za kukaa watazamaji. Lengo ni kuwajengea washiriki uzoefu wa kufanya uchunguzi kabla ya tukio na kutambua mapema hali yoyote inayohitaji hatua zaidi.
Profesa Najat amesema mazoezi hayo yatasaidia kutathmini uwezo uliopo na kubaini maeneo yanayohitaji kuendelea kuimarishwa katika kipindi kilichobaki kuelekea AFCON 2027.
Amesema, hata hivyo, maandalizi hayo hayaishii katika AFCON pekee kwa sababu utaalamu, vifaa na mifumo ya ushirikiano inayojengwa sasa itabaki kuwa sehemu ya uwezo wa Taifa katika kusimamia usalama wa matukio mengine makubwa yatakayofanyika nchini.
“Uwezo tunaoujenga kupitia warsha hii utakuwa rasilimali ya kudumu kwa Taifa letu na utatumika katika kulinda mikutano ya kimataifa, mashindano ya michezo, ziara za viongozi, mikusanyiko mikubwa ya kitaifa na matukio mengine yenye umuhimu mkubwa kwa nchi,” amesema Profesa Najat.
Ameongeza kuwa moja ya mambo yanayotarajiwa baada ya warsha hiyo ni kuwa na mwelekeo wa pamoja kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kipindi kilichobaki kuelekea AFCON 2027, huku kila taasisi ikifahamu eneo lake la wajibu na namna ya kushirikiana na taasisi nyingine.
Profesa Najat ameishukuru IAEA kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kujenga uwezo wa wataalamu na kuimarisha mifumo ya usalama wa nyuklia, akisema ushirikiano huo umekuwa muhimu katika kupata utaalamu, mafunzo na uzoefu unaohitajika katika kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Wataalamu kutoka IAEA, Lacina Saro, amepongeza Tanzania kwa kuanza mapema maandalizi ya usalama wa nyuklia kuelekea AFCON 2027, akisema tukio kubwa la aina hiyo linahitaji mipango ya kina, mafunzo na mazoezi ya kutosha kabla ya kuanza kwa mashindano.
“Uchaguzi wa Tanzania kuwa miongoni mwa wenyeji wa AFCON 2027 ni jambo la kujivunia, lakini pia unaambatana na wajibu. Mpangilio wa usalama wa nyuklia wa kiwango hiki unapaswa kuandaliwa mapema, kufanyiwa majaribio kwa kina na kutekelezwa kwa ufanisi na timu za kitaifa zilizopewa mafunzo,” amesema Saro.
Amesema IAEA itaendelea kushirikiana na Tanzania kupitia utoaji wa miongozo, mafunzo na msaada wa kiufundi unaolenga kuimarisha uwezo wa nchi katika usalama wa nyuklia.
“Tuko hapa kufanya kazi pamoja nanyi na kuunga mkono Tanzania katika kujenga uwezo wa usalama wa nyuklia ambao mnaweza kuutegemea wakati wa AFCON 2027 na hata baada ya mashindano hayo,” amesema Saro.
Naye Mkurugenzi wa Teknolojia na Huduma za Ufundi wa TAEC, Dkt. Remigius Kawala, amesema Tanzania inaendelea kujiandaa katika eneo la usalama wa nyuklia na mionzi huku Serikali ikiendelea kuwekeza katika wataalamu, vifaa na mifumo inayohitajika kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika katika mazingira salama.
Dkt. Kawala amesema Tanzania ina wataalamu wenye ujuzi pamoja na vifaa vinavyoweza kutumika katika kubaini na kukabiliana na vitisho vinavyoweza kuhusisha mionzi, huku mafunzo yanayoendelea yakilenga kuongeza uwezo wa taasisi mbalimbali kufanya kazi kwa pamoja.
Amesema maandalizi hayo yanalenga pia kujenga uwezo wa muda mrefu utakaotumika kulinda wananchi na miundombinu muhimu wakati wa matukio mengine makubwa yatakayofanyika nchini.
Dkt. Kawala amewataka washiriki kutumia kikamilifu fursa ya mafunzo hayo kuongeza ujuzi, kubadilishana uzoefu na kuimarisha uratibu baina ya taasisi zao, hatua ambayo itasaidia kuongeza utayari wa nchi kuelekea mashindano hayo.
Warsha hiyo itahitimishwa Septemba 4, 2026, baada ya washiriki kupitia mafunzo ya darasani na mazoezi ya vitendo yatakayohusisha maandalizi ya eneo, uchunguzi wa kimionzi, tathmini ya tahadhari na namna ya kuchukua hatua pale tukio lisilo la kawaida linapobainika.
TAEC itaendelea kushirikiana na taasisi za kitaifa na washirika wa kimataifa katika kuimarisha usalama wa nyuklia na mionzi nchini, huku maandalizi ya AFCON 2027 yakitumika pia kama fursa ya kuongeza uwezo wa wataalamu na kuimarisha mifumo itakayoendelea kutumika hata baada ya mashindano hayo.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha Tanzania inaingia katika AFCON 2027 ikiwa imejiandaa si katika viwanja na miundombinu pekee, bali pia katika eneo la usalama, ili wananchi na wageni watakaofika nchini waweze kushiriki na kufurahia mashindano hayo katika mazingira salama.