Na. Mwandishi Maalumu – Arusha

31/08/2026 Jumla ya watu 1,005 wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo na macho wakati wa kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika jana mkoani Arusha

Kambi hiyo maalumu ilikuwa ikifanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI–ALMC) na kudhaminiwa na GSM Foundation kwa lengo la kuwafikia wananchi wa Kanda ya Kaskazini na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

Akizingumza wakati wa kufunga kambi hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete – Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (JKCI–ALMC) Dkt. Godwin Kivuyo alisema idadi ya wagonjwa waliopatiwa huduma imevuka lengo lililowekwa hatua inayoonesha mwitikio mkubwa wa wananchi kutumia fursa zilizopo kupata huduma za afya.

“Kambi hii imekuwa na siku tano ambazo tulikuwa tumedhamiria kuona wagonjwa elfu moja angalau wagonjwa kati ya 150 hadi 200 kwa siku, mpaka leo tumeweza kuona wagonjwa 1,005 hivyo kufikia lengo tulilojiwekea”, alisema Dkt. Kivuyo.

Dkt. Kivuyo alisema kupitia kambi hiyo wataalamu wa JKCI – ALMC wameweza kufanya vipimo zaidi ya 800 kuchunguza magonjwa ya moyo na macho.

Kwa upande wake Mratibu kutoka GSM Foundation Julius Ndyakoha alisema GSM kufadhili kambi hiyo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii, kuunga mkono jitihada zinazofanywa na JKCI pamoja na Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini.

Julius alisema GSM Foundation itaendelea kushirikiana na wadau pamoja na taasisi zinazotoa huduma za afya ili kusaidia kufanikisha malengo ya kuongeza fursa ya upatikanaji wa matibabu kwa wananchi.

Leonila Baha mkazi wa Arusha mjini alisema utaratibu wa utoaji wa huduma katika kambi hiyo umesaidia kupunguza muda wa kusubiri licha ya idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza.

“Kambi hii imekuwa na utaratibu mzuri, huduma zimetolewa kwa haraka, wataalamu wa afya walikuwepo wa kutosha na hakukuwa na kujuana ili mtu apate huduma hivyo kila mtu ameondoka akiwa ameridhika na huduma”, alisema Leonila.

Leonia alisema wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kuchunguza afya zao mara kwa mara na kutopuuza fursa za kupata huduma za afya pale zinapojitokeza.