NA DENIS MLOWE, IRINGA 
MWANAFUNZI wa zamani wa Shule ya Sekondari Tosamaganga, Dkt. Greyson Nyamoga, ambaye kwa sasa ni Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), amewataka wanafunzi waliowahi kusoma katika shule hiyo kuendelea kuirejeshea jamii kwa kuchangia maendeleo ya taasisi hiyo.
Dkt. Nyamoga amesema hatua yake ya kushiriki katika harakati za kuchangia upatikanaji wa basi la shule hiyo imetokana na kutambua mchango mkubwa ambao shule hiyo iliutoa katika safari yake ya elimu na maisha yake ya sasa.
Amesema akiwa mmoja wa Wanafunzi waliopita katika shule hiyo, anaamini mafanikio ambayo ameyafikia leo hayawezi kutenganishwa na msingi wa elimu alioupata shuleni hapo.
Dkt. Nyamoga ni Mdau wa Elimu kwa nafasi yake ya Mhadhiri mwandamizi katika Chuo cha SUA, jambo ambalo limemfanya kuona umuhimu wa wanafunzi wa zamani kutumia nafasi na mafanikio waliyonayo kusaidia kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi wanaosoma shuleni hapo.
Amesema mpango wa kuchangia basi ni sehemu ya jitihada za Wanafunzi wa zamani kuendelea kuwa karibu na shule yao na kuhakikisha wanafunzi wa sasa wanapata mazingira bora zaidi ya kujifunzia na kushiriki shughuli mbalimbali za kielimu.
Dkt. Nyamoga, ambaye pia amekuwa mdau mkubwa wa maendeleo amekuwa na mchango mkubwa katika tamasha la Lusinga Day linalofanyika kila mwaka mwezi Desemba mwishoni katika Kijiji cha Lusinga, Kata ya Dabaga, Wilaya ya Kilolo, likiwa na lengo la kuimarisha mshikamano wa wananchi na kuchochea juhudi za maendeleo katika Kijiji hicho na Wilaya ya Kilolo kwa ujumla.
Dkt Nyamoga alisema kuwa basi hilo linatarajiwa kuwa msaada mkubwa kwa shule, hasa katika kurahisisha usafiri wa wanafunzi wanapokuwa na shughuli za kielimu nje ya shule, mashindano mbalimbali ya Kitaaluma na Michezo, ziara za kielimu na shughuli nyingine zinazohitaji usafiri.
Ameeleza kuwa mchango wa wanafunzi wa zamani haupaswi kuishia kwenye basi pekee, bali uwe mwanzo wa kujenga utamaduni wa alumni kuendelea kuisaidia shule yao kwa maeneo mbalimbali kulingana na mahitaji yaliyopo.
Dkt. Nyamoga amewahimiza wanafunzi wengine waliowahi kusoma katika shule hiyo kujitokeza na kushiriki katika mpango huo, akisisitiza kuwa maendeleo ya shule ni jukumu linaloweza kufanywa kwa pamoja na kizazi cha zamani pamoja na kizazi cha sasa.
Alisema kuwa mtu yoyote ambaye ataguswa na angependa kuchangia anaruhusiwa kufanya hivyo. Michango yote itumwe kupitia akaunti ya TAO:
Jina la akaunti: *Tosamaganga Alumni Organisation*
Jina la Benki: *CRDB Bank PLC*
Namba ya Akaunti:
 *015c492431600*
Tawi: *Mlimani City*
Dr. Nyamoga amesisitiza kuwa 
uaminifu wao Viongozi wa TAO ni kipaumbele chao na nguzo imara ya kuaminika kwa ALUMNI wote na Jamii kwa ujumla hivyo fedha zote zitakazokusanywa zitakuwa salama kabisa. 
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya maandalizi ya kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Shule hiyo na itasaidia sana kuwafanya wanafunzi wa zamani kuendelea kushirikiana katika kuboresha shule yao, huku wakilenga kuhakikisha kizazi kinachofuata kinapata fursa bora zaidi za elimu na maendeleo.