Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog,Dodoma

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesema kinaendelea kuwa chuo pekee nchini Tanzania kinachomiliki Hospitali ya Rufaa ya Wanyama yenye vifaa vya kisasa vinavyowawezesha wanafunzi wa tiba za wanyama kupata mafunzo kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 31, 2026 Jijini Dodoma, wakati akieleza utekelezaji wa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2026/27, Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael Chibunda, amesema hospitali hiyo ina vifaa mbalimbali vya kisasa vinavyopatikana katika hospitali za binadamu.

Amesema hospitali hiyo ina huduma na vifaa ikiwemo X-ray, ultrasound pamoja na theatre yenye vifaa kwa ajili ya kufanya operesheni, jambo linalowawezesha wanafunzi kupata uzoefu wa vitendo wakati wa mafunzo yao.

“Ni katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo pekee yake nchi hii tuna hospitali ya rufaa ya wanyama. Ukija kuitembelea hospitali yetu, vile vifaa ambavyo unaviona kwenye hospitali za watu, sehemu kubwa na sisi tunavitumia,” amesema Prof. Chibunda.

Ameongeza kuwa uwepo wa mazingira hayo ya kujifunzia unawasaidia wanafunzi wanaosomea udaktari wa wanyama kuhitimu wakiwa na uwezo unaokubalika kimataifa.

Prof. Chibunda amesema ubora wa SUA umeendelea kuvuka mipaka ya Tanzania, hali inayothibitishwa na uwepo wa wanafunzi kutoka nje ya nchi wanaokuja kusoma katika chuo hicho kutokana na umahiri wake katika sekta za kilimo na mifugo.

Amesema kwa mwaka huu, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imewadhamini vijana kutoka Burundi na Benin kusoma katika sekta za kilimo na mifugo, huku benki hiyo ikiwaelekeza kusoma Tanzania katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

“Bank ndio iliwapa wao maelekezo kwamba hao wanafunzi waende wakasome Tanzania Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, kati ya vyuo vyote vilivyopo Afrika,” amesema.

Aidha,Prof. Chibunda amesema SUA kwa sasa ina jumla ya wafanyakazi 1,558 walio kwenye payroll ya Serikali, ambapo takribani 600 ni wanataaluma.

Amesema idadi hiyo ya wanataaluma inaifanya SUA kuwa katika nafasi nzuri kwa kuzingatia uwiano kati ya idadi ya wanafunzi na walimu, jambo ambalo pia huzingatiwa katika upangaji wa viwango vya vyuo vikuu duniani.

Amesema Serikali imeendelea kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa wafanyakazi chuoni hapo, ambapo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita SUA ilipata kibali cha kuajiri wafanyakazi wapya takribani 270, wengi wao wakiwa wanataaluma.

“Napenda kuchukua nafasi hii kushukuru sana Serikali ya Mama Samia. Sasa hivi tatizo la wafanyakazi sisi limepungua sana,” amesema.

Prof. Chibunda amesema baada ya kupungua kwa changamoto ya wafanyakazi, SUA sasa inakabiliwa zaidi na hitaji la kuwaendeleza kielimu baadhi ya waajiriwa wapya, hususan wanataaluma wenye shahada za kwanza.

Amesema kwa mujibu wa mahitaji ya taaluma ya ualimu wa vyuo vikuu, wanataaluma wanapaswa kuendelea na masomo ya uzamili na hatimaye PhD ili kufikia viwango vinavyohitajika kufundisha katika elimu ya juu.

Amesema SUA tayari imeanza mchakato wa kuwawezesha baadhi ya wanataaluma hao kuendelea na masomo ndani ya chuo, huku ikishirikiana na wadau mbalimbali kutafuta nafasi kwa wengine kusoma nje.

“Kwa hiyo tunaendelea na mchakato wa kuwasomesha. Kuna baadhi ambao wameanza kusoma pale pale chuoni, lakini na wengine tunatafuta nafasi kupitia wadau wetu mbalimbali kwa ajili ya kuwapata nafasi ya kwenda kusoma ili nao wapate level ya elimu ambayo tunaitegemea kwa ajili ya kuja kutoa mafunzo,” amesema Prof. Chibunda.