Na Happy Lazaro, Arusha
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha imevuka lengo la makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 baada ya kukusanya Sh520 bilioni dhidi ya lengo la Sh504.7 bilioni.
Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha, Deogratius Shuma, amesema makusanyo hayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 103, huku yakiongezeka kwa asilimia 9.69 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Shuma alisema ongezeko hilo ni sawa na zaidi ya Sh25 bilioni, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya TRA, walipa kodi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali.
Ameyasema hayo katika hafla ya kuwapongeza walipa kodi na wadau wa TRA mkoani Arusha,a ambapo amesema utayari wa wafanyabiashara kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi, sambamba na huduma bora zinazotolewa na watumishi wa TRA, umechangia kwa kiasi kikubwa kufikia mafanikio hayo.
“Mafanikio haya yasingewezekana bila ushirikiano na utayari wa walipa kodi kulipa kodi, pamoja na watumishi wa TRA kutoa huduma bora kwa walipa kodi na wadau wanaofika kupata huduma,” amesema.
Shuma amesema TRA Arusha pia imeanza mwaka wa fedha 2026/2027 kwa kasi, baada ya mwezi Julai kukusanya Sh49.82 bilioni dhidi ya lengo la Sh42.69 bilioni.
Ameongeza kuwa , makusanyo hayo ni ziada ya Sh7.2 bilioni, sawa na ufanisi wa asilimia 116.
“Tumeweza kuanza vyema na tunaendelea kutoa shukrani kwa walipa kodi na watumishi wote ambao wamefanya kazi kwa bidii, uelewa, uaminifu na uadilifu mkubwa,” amesema.
Aidha, Shuma amewapongeza wafanyabiashara na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wanaoupa TRA katika kuongeza makusanyo ya Serikali.
Amevitaja vyama vya wafanyabiashara na wadau wa sekta ya utalii ikiwamo TATO, TLTO, TTGA na TAUTO, pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania na AKIBOA.
30
Amefafanua kuwa, ushirikiano huo umekuwa muhimu katika kujenga uelewa kuhusu ulipaji kodi na kuhakikisha wafanyabiashara wanatimiza wajibu wao kwa Serikali.
Shuma pia amewatambua watumishi wa TRA kuwa sehemu muhimu ya mafanikio hayo, akisema bidii, uaminifu na uadilifu wao katika kuwahudumia walipa kodi umechangia kuimarisha makusanyo.
Ameongeza kuwa ,TRA itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wafanyabiashara na wadau wengine ili kuimarisha ulipaji kodi, kuboresha huduma na kuongeza mapato ya Serikali.

