NA DENIS MLOWE IRINGA 

MEYA wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, amesema utalii ni biashara yenye uwezo mkubwa wa kuchochea uchumi na kuunda ajira kwa vijana, akiwataka wananchi kutumia fursa zilizopo katika vivutio vya utalii vya mkoa huo.

Ngwada aliyasema hayo wakati akiwaaga wananchi zaidi ya 70 wanaoshiriki ziara ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Iringa, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ziara iliyoandaliwa na taasisi ya Iringa Safari Hub.

Amesema Manispaa ya Iringa imebahatika kuwa sehemu muhimu ya utalii katika Nyanda za Juu Kusini, hivyo wananchi, hususan vijana, wanapaswa kutumia fursa hiyo kujifunza na kujiandaa kushiriki katika shughuli za utalii.

“Utalii ni biashara wenzetu wa maeneo ya Arusha na maeneo mengine wanajenga, wanaishi, wanatibu wazazi wao na wanajitibu wao kupitia utalii na Serikali yetu inafanya jitihada kubwa kuhakikisha inakuza utalii katika maeneo ya kusini,” alisema Ngwada.

Alisema Iringa imekuwa kitovu cha utalii katika Nyanda za Juu Kusini, huku akieleza kuwa uwekezaji unaoendelea katika maeneo mbalimbali ukiwemo Kihesa-Kilolo unatarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi na ajira zinazotokana na sekta hiyo.

Ngwada alisema kuwa ongezeko la shughuli za utalii litahitaji wataalamu mbalimbali, wakiwemo waongoza watalii, madereva wa magari ya kitalii pamoja na wafanyabiashara watakaowekeza katika usafirishaji wa watalii.

“Tunatumaini tour guide watatoka humu, tunaamini madereva ambao wataendesha magari ya kitalii watatoka humu tunaamini pia wafanyabiashara watakaonunua magari ya utalii watatoka miongoni mwa vijana wa Manispaa ya Iringa,” alisema.

Aidha, Ngwada amepongeza Iringa Safari Hub kwa kuandaa ziara hiyo, akisema safari za pamoja zinatoa fursa kwa wananchi wengi kutembelea vivutio vya utalii kwa gharama nafuu huku zikiongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuvilinda na kuvitangaza.

Kwa upande wake, Meya Mstaafu wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe, ameipongeza Iringa Safari Hub kwa kuandaa ziara hiyo na kumshukuru Meya Ngwada kwa kusaidia kundi hilo kupata fursa ya kutembelea baadhi ya vituo vya utalii bila kulipia kiingilio.

Kimbe amesema taasisi hiyo ina nafasi kubwa ya kuchochea ajira kwa vijana endapo itaendelea kuimarika na kusajiliwa rasmi katika shughuli za utalii.

Ameitaka taasisi hiyo kufikiria kuwa na magari yake ya kitalii yatakayoweza kutumika kusafirisha watalii, jambo ambalo alisema litafungua ajira kwa madereva na waongoza watalii.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Iringa Safari Hub, Emmanuel Jasper Mgavilwa, amesema taasisi hiyo imeanzisha utaratibu wa kuwaunganisha wananchi katika safari za utalii kwa lengo la kupunguza gharama na kuwawezesha watu wengi zaidi kufurahia vivutio vya utalii.

Mgavilwa amesema safari hiyo imehusisha zaidi ya watu 70 na kwamba mshiriki hulipa shilingi 90,000 ambazo zinahusisha usafiri, kiingilio, malazi, chakula na mahitaji mengine muhimu ya safari.

Amesema utaratibu huo umeongeza mwamko kwa wananchi, kwa kuwa mtu anayesafiri peke yake au na familia anaweza kutumia zaidi ya shilingi 500,000 hadi 600,000 kwa safari kama hiyo.

Ameongeza kuwa mbali na Ruaha, safari hiyo pia inatoa fursa kwa washiriki kutembelea vivutio mbalimbali vya kihistoria na kiutamaduni vya Iringa, ikiwemo Kihesa-Kilolo, Jiwe la Igeleke, Jiwe la Gangilonga, Kitanzini na Kalenga ambako kuna historia ya Chifu Mkwawa.

Kwa upande wake, Mlezi wa Iringa Safari Hub, Nguvu Chengula, amewapongeza washiriki kwa uamuzi wao wa kutembelea vivutio vya utalii, akisema safari hizo hazihusu burudani pekee bali pia hutoa fursa ya kujifunza, kujenga mahusiano na kupunguza msongo wa mawazo.

Chengula amesema kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni sehemu ya kuitangaza na kuienzi hifadhi hiyo ambayo ni fahari kwa Mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla.

Amewataka washiriki kusafiri kwa amani na kurejea salama huku wakiwa na uzoefu mpya na maarifa yatakayowasaidia kuendelea kuhamasisha wananchi wengine kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.