Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog,Dodoma
Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeeleza kuwa hatua mbalimbali za kudhibiti visumbufu na magonjwa ya mimea imechangia kuimarisha uzalishaji na usalama wa chakula nchini, huku tani zaidi ya milioni moja za mazao zikiokolewa dhidi ya uharibifu wa ndege aina ya kolea katika mwaka wa fedha 2025/26.
Akizungumza Agosti 27,2026 na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Nduguru, amesema mamlaka hiyo imeendelea kutumia teknolojia za kisasa katika kukabiliana na visumbufu na magonjwa yanayotishia uzalishaji wa mazao.
Profesa Nduguru amesema ndege aina ya kolea wapatao milioni 233 walivamia wilaya 21, ambapo mamlaka iliweza kuchukua hatua za udhibiti na kuokoa takribani tani milioni moja za mazao ya nafaka, ikiwemo mtama na mpunga.
“Tunapozungumzia visumbufu, maana yake ni magonjwa na wadudu waharibifu ambao wangeweza kuathiri uzalishaji wa mazao yetu,” amesema Profesa Nduguru.
Amesema TPHPA pia ilidhibiti milipuko ya viwavijeshi katika halmashauri 52 zilizoathirika, ambapo shughuli hizo zilifanyika kwa kushirikiana na wakulima na kutumia viwakilifu vilivyotolewa kwa ruzuku.
Profesa Nduguru,. amebainisha Kuwa udhibiti huo ulifanyika katika eneo lenye ukubwa wa ekari 28,500 na uliwezesha kuokoa takribani tani 342,787 za mazao mbalimbali, yakiwemo mahindi na mazao mengine ya chakula.
Aidha, amesema mamlaka ilifanya udhibiti wa visumbufu katika maeneo mbalimbali yaliyoathirika, ikiwemo maeneo yenye uvamizi wa nzige, huku teknolojia ya kisasa ikitumika kubaini aina halisi ya visumbufu na kuchagua njia sahihi ya udhibiti.
Amesema katika eneo la Kwako, awali ilidhaniwa kuwa nzige waliovamia walikuwa nzige wekundu, lakini baada ya wataalamu kuchukua sampuli na kufanya uchunguzi wa kisasa, ilibainika kuwa walikuwa nzige wa aina ya Tree Locust, hatua iliyowezesha mamlaka kutumia dawa maalumu kwa usahihi na hata drones katika udhibiti.
Aidha, amebainisha Kuwa THPA imepiga hatua katika uchunguzi wa magonjwa ya mimea kwa kutumia teknolojia ya DNA na njia nyingine za kisasa, jambo lililosaidia kubaini vimelea vilivyokuwa vikisababisha kuoza kwa mazao kama nyanya, vitunguu, karoti na pilipili hoho.
“Baada ya kujua aina ya vimelea vilivyokuwa vinaathiri mazao yale, tulipanga mkakati wa pamoja wa namna ya kudhibiti visumbufu vile kwa kutumia kiwakilishi sahihi,” amesema.
Katika upande wa masoko ya kimataifa, Profesa Nduguru amesema TPHPA imeendelea kuwezesha wafanyabiashara wa Tanzania kupata masoko mapya kwa kuhakikisha mazao yanakidhi viwango vya afya ya mimea vinavyotakiwa na nchi zinazoagiza.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, kampuni nane mpya za Tanzania ziliruhusiwa kusafirisha parachichi kwenda China baada ya kutimiza matakwa ya soko hilo, na hivyo kufanya jumla ya kampuni za Tanzania zilizopewa kibali kufikisha 24.
Ameongeza kuwa TPHPA kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau wengine imewezesha usajili wa kampuni 444 za Tanzania katika mfumo wa forodha wa China, maarufu kama GACC, kwa ajili ya kusafirisha mazao mbalimbali kwenda nchini humo.
Profesa Nduguru amesema hatua hizo zinafungua fursa kubwa kwa vijana na wadau wa kilimo kujikita zaidi katika kilimo-biashara, akibainisha kuwa China ni soko kubwa lenye watu zaidi ya bilioni 1.4.
Amesema TPHPA pia imefanikisha kufunguliwa kwa masoko mapya katika nchi mbalimbali, ikiwemo Ushelisheli kwa mazao kama kabichi, viazi, vitunguu saumu, tangawizi, kitunguu maji na mimea ya viungo.
Kwa upande mwingine, amesema mamlaka imeendelea kulinda masoko yaliyopo kwa kuhakikisha Tanzania inatimiza matakwa ya nchi inazofanya nazo biashara, akitoa mfano wa hatua zilizochukuliwa kuthibitisha kwa Umoja wa Ulaya kuwa Tanzania haina bakteria aina ya Xylella fastidiosa
Amesema TPHPA ilizunguka maeneo mbalimbali nchini na kukusanya sampuli 5,664 za mimea kwa ajili ya uchunguzi wa kisasa, na matokeo yalionyesha kuwa bakteria huyo hakuwapo nchini. Taarifa hiyo iliwasilishwa kwa Umoja wa Ulaya Juni 13, 2025 na Tanzania kuruhusiwa kuendelea kufanya biashara katika soko hilo.
Profesa Nduguru amesema mafanikio hayo yanaonyesha mchango wa TPHPA katika kulinda uzalishaji wa chakula, afya ya mimea na kuongeza fursa za masoko ya kimataifa, huku akibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26 mamlaka pia ilichangia kufunguliwa kwa masoko ya mazao ya Tanzania nchini Afrika Kusini, India, China, Misri na Ushelisheli.
