
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ametoa rai kwa wazazi na walezi mkoani humo kuhakikisha watoto walio chini ya umri wa miaka 10 wanapata chanjo ya polio ya matone aina ya nOPV2, itakayotolewa kuanzia Agosti 27 hadi 30, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na timu ya kampeni ya chanjo mkoani humo, Agosti 24, 2026, Kunenge amesema Serikali inafanya jitihada kubwa kuboresha afya za watoto na ustawi wa jamii.
Amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuepuka upotoshaji kuhusu chanjo ili kulinda watoto dhidi ya madhara makubwa ya ugonjwa wa polio, ikiwemo ulemavu na kupoteza maisha.
Kunenge amesema Mkoa wa Pwani umejiandaa kikamilifu kuhakikisha kampeni hiyo inafanyika kwa ufanisi.
Aidha ameeleza kuwa jumla ya watoto 587,509 walio chini ya umri wa miaka 10 mkoani Pwani wanatarajiwa kupatiwa chanjo hiyo katika awamu ya pili ya kampeni ya chanjo ya polio, ikiwa ni sehemu ya watoto milioni 6.5 wanaolengwa katika mikoa nane nchini.
Kunenge amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka kipaumbele katika afya na ustawi wa Watanzania, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa chanjo, dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Aliwataka viongozi wa Serikali, viongozi wa madhehebu ya dini, jamii na wadau mbalimbali kushirikiana katika kuhamasisha wananchi na kuhakikisha watoto wote wanaostahili wanapata chanjo hiyo.
Amesema chanjo zinazotolewa nchini zinazingatia viwango vya usalama na ubora, zimeidhinishwa na mamlaka husika za afya na hutolewa kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa.
Kunenge amesema chanjo ya nOPV2 ni salama na hutolewa mahsusi kupitia kampeni za chanjo kwa lengo la kuzuia maambukizi ya polio, na kwamba si sehemu ya ratiba ya kawaida ya chanjo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Pwani, Alfred Ngoi, amesema chanjo hiyo itatolewa nyumba kwa nyumba, katika vituo vya kutolea huduma za afya, zahanati na hospitali, pamoja na shuleni na maeneo yenye mikusanyiko ya watu, ikiwemo masoko, stendi na nyumba za ibada.
Ameeleza kuwa ugonjwa wa polio unasababishwa na virusi vya polio, ikiwemo aina ya wild poliovirus type 1, vinavyoweza kumsababishia mtoto kupooza na hata kupoteza maisha, huku akisisitiza kuwa ugonjwa huo unaweza kuzuilika kwa chanjo.
Kampeni hiyo itahusisha mikoa nane ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Dodoma na Mara huku awamu nyingine ya kampeni hiyo inatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 2, mwaka huu.
