Wagonjwa watano wenye matatizo ya mishipa ya damu ya moyo iliyoziba (coronary artery disease) wamefanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo bila kusimamisha moyo (off Pump CABG).
Upasuaji huo umefanyika katika kambi maalumu ya siku tano iliyofanywa na watalaamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Jaslok iliyopo Mumbai nchini India.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kufunga kambi hiyo jijini Dar es Salaam daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Alex Joseph alisema wagonjwa hao wamefanyiwa upasuaji kwa mafaniko makubwa.
“Tunawashukuru hospitali za rufaa kwa kuleta wagonjwa kwani upasuaji umefanyika kwa ufanisi na wagonjwa wote wanaendelea vizuri na matibabu ambapo wakati wowote tutawaruhusu kurejea nyumbani”, alisema dkt. Alex
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka Hospitali ya Jaslok iliyopo Mumbai nchini India Upendra Bhalerao alisema watu wenye matatizo ya mishipa ya damu wanapswa kufika katika taasisi hiyo ili waweze kupatiwa matibabu mapema.
“Hii ni mara yangu ya tatu kufanya upasuaji wa namna hii hapa JKCI, na umekuwa ukifanyika kwa ufanisi mkubwa hivyo niwaombe watu wote ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi vizuri kutokana na matatizo ya mishipa ya damu ya moyo kuziba wafike JKCI ili wapatiwe matibabu ya kisasa”, alisema Dkt. Bhalerao.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Health and Wellness Companion LTD Dkt. Priyank Punatar alisema Taasisi hiyo imekuwa ikiwaleta watalaamu kutoka nchini India hivyo kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kuwasafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi.
“Namshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani amekuwa akisogeza huduma za matibabu ya kibingwa karibu na wananchi wasiokuwa na uwezo wa kwenda kutibiwa nje ya nchi”, alisema Punatar.
Ushirikiano kati ya JKCI na wataalamu kutoka Hospitali ya Jaslok unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa za moyo na mishipa ya damu nchini pamoja na kuongeza fursa kwa wagonjwa kupata matibabu ndani ya Tanzania.
