Na John Walter -Babati 

Shirika la WaterAid Tanzania limetoa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Shilingi milioni 4.29 kwa Kikundi cha Mabingwa cha Kijiji cha Sangara, Kata ya Riroda, Wilaya ya Babati, kwa ajili ya kuwawezesha kufanya shughuli za kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Vifaa hivyo vimetolewa kupitia Mradi wa BASIN (Behavioral Adaptation for Water Security and Inclusion), unaotekelezwa na WaterAid Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kuimarisha usalama wa maji na kuchochea mabadiliko chanya ya tabia katika jamii.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, amesema moja ya malengo makuu ya mradi huo ni kuongeza usalama wa maji na kuhakikisha jamii zilizo katika hatari ya kukosa huduma ya maji kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinajumuishwa katika juhudi za kutafuta suluhisho.

Amesema kupitia Mabingwa wa Kubadilisha Tabia katika jamii, wananchi wataendelea kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji.

“Mabingwa hawa wana nafasi kubwa ya kusaidia jamii kubadilisha tabia, kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Mzinga.

Aidha, Mzinga ameiomba jamii kuacha tabia zinazochangia uharibifu wa mazingira, akieleza kuwa uharibifu wa mazingira una athari kubwa ikiwemo kuathiri upatikanaji wa maji.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Riroda, Nyangweli, amelishukuru WaterAid Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutunza mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kikundi hicho cha Mabingwa, chenye jumla ya wanachama 14, kimeahidi kutumia nafasi hiyo kuwa chombo muhimu cha kuelimisha na kuunganisha jamii katika masuala ya utunzaji wa mazingira, uhifadhi wa vyanzo vya maji na matumizi bora ya rasilimali za maji.

Naye Dickson Matei, Afisa Maendeleo Mwandamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, ameahidi kusimamia matumizi sahihi ya vifaa vilivyotolewa ili viweze kutumika kutekeleza malengo yaliyokusudiwa.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali, WaterAid na jamii ni muhimu katika kuhakikisha jitihada za kulinda mazingira na kuimarisha usalama wa maji zinaendelea kuwa endelevu.