Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
ALIYEWAHI kuwa kocha wa klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam, David Mwamwaja amefariki dunia Alfajiri ya leo katika hospitali ya Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya familia ya marehemu, Mwamwaja alikuwa amelazwa kwa matibabu Muhimbili kabla ya umauti kumkuta Alfajiri ya leo.
Taarifa hiyo imesema kwamba mwili wa marehemu Mwamwaja aliyewahi pia kufundisha klabu za Bandari ya Mtwara, AFC ya Arusha, Tanzania Prisons na JKT Tanzania unatarajiwa kusafirishwa leo kupelekwa Kyela, mkoani Mbeya kwa mazishi.
Mwamwaja ambaye enzi zake alikuwa kiungo wa klabu ya Kurugenzi ya Arusha na timu ya mkoa huo, Meru Worriors mwaka 1999 alichukuliwa na Simba SC kuunda kikosi cha timu hiyo baada ya wakongwe wengi kuondoka na wengine kuachwa.
Ndiye aliyewasajili wachezaji wengi chipukizi kama akina Athumani Machuppa, Mrisho Moshi, Prosper Omella, Wilfred Kidau, Henri Freeman, Thabit Mjengwa, Edward Kayoza na wengine akishirikiana na kocha mwingine muumini wa soka ya vijana, Ramadhani Aluko.
Hata hivyo, Mwamwaja hakudumu Simba SC kwa pamoja na Aluko na aliyekuwa Meneja wa timu, Hassan Chabruma walifukuzwa na ndipo akaajiriwa kocha Mrundi, Nzoyisaba Tauzany (sasa merehemu pia).
Mungu ampumzishe kwa amani kocha Mwamwaja. Amin.