Bunifu mbalimbali kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) zimeendelea kuwavutia wanafunzi na wananchi wanaotembelea banda la chuo hicho katika Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika Shule ya Sekondari Usagara, Tanga.

Wageni wanaendelea kupata fursa ya kujionea na kujifunza kuhusu bunifu zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya afya na maeneo mengine ya kijamii.

Miongoni mwa bunifu hizo ni Robospine, kifaa cha roboti kinachosaidia watoto wenye spina bifida kusimama, kutembea na kufanya mazoezi, huku kikifuatilia maendeleo yao ya tiba. Bunifu hii imebuniwa na Alexander Tilya.

BiliMeasure ni kifaa kinachopima na kuwezesha ufuatiliaji endelevu wa kiwango cha bilirubini kwa watoto wachanga wenye manjano bila kuhitaji kuchomwa sindano au kuchukuliwa damu wakati wa matibabu kwa kutumia kifaa cha phototherapy. Bunifu hii imebuniwa na Abubakar Victor.

Siku Smart ni kifaa cha kielektroniki kinachotumika kutabiri mzunguko wa hedhi na kipindi cha yai kupevuka bila kuhitaji programu za rununu au ujuzi wa kidijitali. Teknolojia hii inalenga kuwasaidia wasichana na wanawake wanaoishi katika maeneo yenye upatikanaji mdogo wa simu janja na intaneti. Bunifu hii imebuniwa na TulinaveAroha Charity.

Bridging Silence ni mradi wa kiteknolojia unaolenga kupunguza changamoto za mawasiliano kati ya watu wanaotumia lugha ya alama na watu wasioifahamu. Mradi huu unatumia Akili Bandia kutambua lugha ya alama na kuibadilisha kuwa maandishi na sauti ya Kiswahili. Bunifu hii imebuniwa na Junior Marandu.

Biosafe ni kiuatilifu hai cha asili kinachoweza kudhibiti vimelea vya magonjwa ya mimea kwa lengo la kuongeza wingi na ubora wa chakula. Kinaweza kutumika katika kilimo hai (organic farming) na kilimo cha kawaida (conventional farming). Kimeundwa kulenga vimelea maalumu vya magonjwa ya mimea, hivyo viumbe wengine wasiolengwa hubaki salama.

Matumizi yake hupunguza utegemezi wa viuatilifu vya kemikali, hivyo kusaidia kupunguza mkusanyiko wa kemikali hatarishi katika mazingira na kulinda afya za watumiaji. Bunifu hii imebuniwa na Zaituni Msengwa.

MoyoGuard ni kifaa cha mkononi kinachorekodi mapigo ya moyo kwa haraka ndani ya sekunde 30 bila kuhitaji intaneti.
Teknolojia yake huchanganua mapigo ya moyo na kumsaidia mtumiaji kuelewa hali ya moyo wake, kutambua mabadiliko yasiyo ya kawaida na kuchukua hatua mapema. Bunifu hii imebuniwa na Staphod Mwahalende.

QR Dharura ni msimbo wa QR unaoweza kuwekwa kwenye begi la shule, stika ya helmeti au kamba ya mkononi ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu za mtu wakati wa dharura. Bunifu hii imebuniwa na Pharm Flavian Sanga.

Maadhimisho hayo yanaendelea hadi 24 Agosti 2026, huku MUHAS ikiendelea kuhamasisha vijana kuhusu umuhimu wa elimu, ujuzi, ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kutatua changamoto zinazozikabili jamii.