Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha leo 
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba akizungumza kwenye mkutano huo
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za ukaguzi, mapambano dhidi ya rushwa na udhibiti wa manunuzi ya umma katika kuzuia upotevu wa rasilimali za Serikali na kukabiliana na utakatishaji fedha.
Ofisi ya CAG ina jukumu la kufanya ukaguzi unaolenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilimali za umma.
Ameyasema hayo leo jijijini Arusha wakati akizungumza katika mkutano wa mwaka wa 19 wa INTOSAI Working Group on the Fight Against Corruption and Money Laundering (WGFACML) ulioandaliwa na Ofisi ya Taifa ya ukaguzi (NAOT).
Kichere amesema mapambano dhidi ya rushwa na uhalifu wa kifedha yanahitaji taasisi mbalimbali kufanya kazi kwa pamoja badala ya kila taasisi kutekeleza wajibu wake kwa kujitegemea.
Amesema ukaguzi wa Serikali haupaswi kuishia katika kubaini dosari baada ya fedha za umma kutumika, bali unapaswa pia kusaidia kutambua vihatarishi vinavyoweza kusababisha upotevu wa fedha, ubadhirifu na vitendo vya rushwa mapema.
“Ukaguzi wa CAG unahusisha pia kuangalia uzingatiaji wa sheria za bajeti, manunuzi na kodi pamoja na ufanisi wa matumizi ya rasilimali za umma.”amesema Kichere.
“Katika eneo la manunuzi ya umma, CAG ameweka msisitizo kwenye umuhimu wa kuwa na mifumo inayowezesha taarifa sahihi kuhusu kampuni na watu wanaonufaika na shughuli zake kupatikana na kuhakikiwa. “amesema .
Ameongeza kuwa ,hatua hiyo ni muhimu katika kubaini mazingira ambayo kampuni zinaweza kutumika kuficha wahusika halisi wanaonufaika na fedha za Serikali.
Amesema changamoto ya wamiliki fiche wa kampuni inaweza kuathiri uadilifu wa manunuzi ya umma endapo kampuni zinazojitokeza kama washindani katika zabuni zitakuwa na uhusiano wa umiliki au udhibiti unaofichwa.
“Katika mazingira hayo, ushindani unaoonekana unaweza kuwa wa bandia na hivyo kuongeza hatari ya Serikali kupata bidhaa au huduma kwa gharama isiyolingana na thamani yake.”amesema .
Kichere amesisitiza umuhimu wa kubadilishana taarifa kati ya taasisi zinazohusika na usajili wa kampuni, ukaguzi, mapambano dhidi ya rushwa, manunuzi ya umma na mamlaka nyingine za udhibiti.
“Kwa mtazamo huo, taarifa za umiliki wa kampuni zinapounganishwa na taarifa za zabuni, mikataba na miamala ya fedha, zinaweza kusaidia kubaini vihatarishi ambavyo vingekuwa vigumu kugundulika kwa kutumia taarifa za taasisi moja pekee.”amesema .
Amefafanua kuwa matumizi ya teknolojia ni sehemu muhimu ya kuimarisha uwezo wa taasisi za ukaguzi na udhibiti katika kukabiliana na uhalifu wa kifedha. Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi tayari inatumia ukaguzi wa mifumo ya TEHAMA na mbinu za kisasa za ukaguzi katika kutathmini hatari, udhibiti wa ndani na uzingatiaji wa taratibu.
Kwa upande wa ushirikiano wa kitaasisi, CAG amesema taasisi za ukaguzi zinapaswa kuwa na uhusiano wa karibu na vyombo kama TAKUKURU na PPRA ili taarifa zinazobainika wakati wa ukaguzi ziweze kusaidia uchunguzi na hatua za kuzuia rushwa.
“Ushirikiano huo pia unaweza kusaidia kuhakikisha mapendekezo ya ukaguzi hayabaki kwenye ripoti pekee, bali yanafuatiwa na hatua zinazolenga kurekebisha mapungufu yaliyobainika.”amesema .
Amesema lengo kuu ni kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi, uwazi na kwa madhumuni yaliyokusudiwa, huku taasisi zikifanya kazi kwa kuzingatia sheria na viwango vya kimataifa vya ukaguzi. Ofisi ya CAG inaeleza kuwa kazi yake inalenga kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa rasilimali za umma.
“Mkutano huo wa 19 wa siku tatu wa WGFACML umewakutanisha wadau wa taasisi kuu za ukaguzi katika kujadili mchango wao katika mapambano dhidi ya rushwa na utakatishaji fedha.”
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU , Neema Mwakalyelye amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (CAG) katika kudhibiti upotevu wa fedha za umma, hususan katika manunuzi ya umma na kuhakikisha uwazi kuhusu wamiliki wa kampuni.
Amesema uwepo wa sheria imara zinazohusu usajili wa kampuni, uwazi wa wamiliki wa kampuni pamoja na udhibiti wa utakatishaji fedha umeongeza uwezo wa taasisi za Serikali kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma.
Amesema maboresho yaliyofanyika katika sheria za manunuzi ya umma yamekuwa muhimu katika kuimarisha mifumo ya udhibiti wa matumizi ya fedha na mali za Serikali, huku yakiiwezesha TAKUKURU kubaini maeneo yenye vihatarishi vya rushwa katika michakato ya manunuzi na utekelezaji wa mikataba ya umma.
“katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2023 hadi sasa, ushirikiano kati ya TAKUKURU na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi umewezesha kufuatilia fedha zinazokadiriwa kufikia Sh bilioni 19.”amesema Mwakalyelye.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano katika kufanya uchunguzi, ukaguzi maalum pamoja na uwasilishaji wa ushahidi unaosaidia katika mashauri yanayofikishwa mahakamani.
Aidha, ameongeza kuwa, ushirikiano huo una umuhimu mkubwa katika kuhakikisha taarifa zinazobainika wakati wa ukaguzi zinafanyiwa kazi kwa wakati, hasa pale zinapoonyesha viashiria vya ubadhirifu, rushwa au matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma.
Amefafanua kuwa ushirikiano kati ya TAKUKURU, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi na mamlaka zinazohusika na manunuzi ya umma unapaswa kuendelea kuimarishwa ili kuziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali na kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis KwameSimba, amesema ushirikiano wa taasisi za Serikali ni nguzo muhimu katika kuzuia rushwa, utakatishaji fedha na upotevu wa rasilimali za umma unaoweza kujitokeza katika michakato ya manunuzi.
Kwamesimba amesema PPRA inaendelea kushirikiana na taasisi zinazohusika na mapambano dhidi ya rushwa pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (CAG), kwa lengo la kuhakikisha mifumo ya manunuzi ya umma inazingatia misingi ya uwazi, ushindani na sheria.
Amesema PPRA inaweka mkazo katika maeneo matano muhimu ambayo ni ushirikiano kati ya taasisi, utoaji wa taarifa za umiliki fiche wa kampuni, uhakiki wa taarifa kupitia mifumo ya Serikali, uchambuzi wa vihatarishi pamoja na utekelezaji wa sheria.
Amesema matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma (NEST) yameongeza uwezo wa Serikali kuunganisha na kuhakiki taarifa kutoka mifumo mbalimbali, jambo linalosaidia kuchunguza taarifa zinazowasilishwa na wazabuni wakati wa michakato ya zabuni.
Amefafanua kuwa, mfumo huo unaweza pia kusaidia kubaini vihatarishi na mazingira yanayoweza kuathiri ushindani katika zabuni, ikiwemo uwepo wa uhusiano usio wazi kati ya kampuni zinazoshiriki katika mchakato mmoja wa ununuzi.

