Na John Walter-Babati

Historia mpya imeanza kuandikwa mkoani Manyara baada ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kufanya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Kituo cha Michezo cha Kitaifa kilichopo Makatanini, katika Halmashauri ya Mji wa Babati, kwa kampuni ya ubia ya CRBC and Zhonglu Sports JV kutoka nchini China.

Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 29 unalenga kujenga kituo kikubwa cha michezo kitakachokuwa na miundombinu mbalimbali ya michezo pamoja na hosteli kwa ajili ya wanamichezo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Tobias Abwao, amesema mradi huo ni fursa kubwa kwa wilaya ya Babati na Mkoa wa Manyara kwa ujumla, huku akitoa shukrani kwa BMT pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuhakikisha kituo hicho kinajengwa Babati.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msita, amesema mradi huo umekuwa ukipangwa kwa muda mrefu na kwa sasa umeingia katika hatua ya utekelezaji.

Amesema kituo hicho kitakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania, hususan wanamichezo, kwa kuwa kitatoa mazingira bora ya mafunzo na kuwa na miundombinu ya michezo ya aina mbalimbali pamoja na hosteli.

Afisa Michezo wa Mkoa wa Manyara, Samwel Pastory, amesema eneo lililochaguliwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ni sahihi na linafaa kwa shughuli za mafunzo na maendeleo ya michezo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Shabani Mpendu, amesema kituo hicho kitakuwa miongoni mwa miradi mikubwa na ya kuvutia katika Jiji/Mji wa Babati, huku akieleza kuwa uwekezaji wake unafikia shilingi bilioni 29.

Akizungumza kwa niaba ya kampuni ya CRBC and Zhonglu Sports JV, Mkandarasi kutoka China, Li Wenzhu, ambaye ni Business Manager wa kampuni hiyo, amesema wamejipanga kuanza kazi mara moja na wanaamini watapata ushirikiano kutoka kwa Serikali na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mshauri elekezi wa mradi huo Beno Batinamani, ujenzi wa kituo hicho utafanyika kwa awamu tatu ndani ya kipindi cha miaka mitatu. 

Ujenzi umeanza rasmi Agosti 14, 2026, na unatarajiwa kukamilika Agosti 14, 2029.

Kukamilika kwa kituo hicho kunatarajiwa kuongeza fursa za mafunzo, kukuza vipaji na kuimarisha maendeleo ya michezo nchini, huku Babati ikijiweka katika nafasi muhimu zaidi katika sekta ya michezo Tanzania.