Mfanyabiashara Hersi Warsame Mohamed  (kushoto) akizungumza kwa furaha na wananchi waliohusika katika mgogoro wa madai ya kudhulumiwa ardhi  na mfanyabiashara  huyo uliodumu kwa miaka 17 katika eneo la Mtoni Kizinga wilayani Temeke  jijini  Dar es salaam  baada ya mgogoro huo kumalizwa kwa njia ya maridhiano na Timu ya Watalaam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Agosti 12, 2026. Wananchi hao ni Bw. Ivan Ruben Kihiyo, Hamisi A. Bora, William Abel Makasi, Ramadhani A. Makopa na Sebatian Gervas Rutayuga,  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Msaidizi wa Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya ardhi, Senso Magesa akishuhudia utiaji saini  maridhiano ya mgogoro wa ardhi kati ya Mfanyabiashara Herse Warsame Mohamed (kushoto) na wananchi watano uliodumu kwa miaka 17 katika eneo la Mtoni Mzinga wilayani Temeke jijini Dar es salaam ambao ulimalizwa kwa njia ya maridhiano na Timu ya Watalaam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Agosti 12, 2026.  Wa tatu kushoto ni kiongozi wa Wananchi hao,  Ivan Kihiyo na kulia ni William Abel Makasi. Wananchi wengine  waliohusika katika maridhiano hayo ni  Hamisi A. Bora, Ramadhani A. Makopa na Sebatian Gervas Rutayuga,  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo tarehe 11 Agosti 2026, amerejesha tabasamu kwa
wananchi watano baada ya kufanikisha maridhiano ya mgogoro wa umiliki wa Kiwanja Na. 2013 na 2014, Kitalu “U”, eneo la Mtoni Kizinga, Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam, uliodumu kwa miaka 17 kati ya mfanyabiashara Hersi Warsame Mohamed na
wananchi hao.

Katika mgogoro huo, wananchi hao wakiongozwa na Bw. Ivan Kihiyo, walimwandikia barua
Mheshimiwa Waziri Mkuu wakilalamika kuwa mfanyabiashara Hersi Warsame Mohamed
amejimilikisha eneo lao kinyume cha sheria. Wananchi hao walimuomba Waziri Mkuu
awasaidie kutatua mgogoro huo.

Timu ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotumwa na Waziri Mkuu kutatua mgogoro
huo, ikiongozwa na Mwenyekiti ambaye pia ni Msaidizi wa Waziri Mkuu – Mahusiano, Asasi
za Kiraia na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bw. Tryphone Mkolokoti, na Katibu wake
ambaye pia ni Msaidizi wa Waziri Mkuu – Masuala ya Ardhi, Bw. Senso Magessa, ilifanikiwa kufanikisha maridhiano hayo kwa kuzingatia taarifa ya uchunguzi wa mgogoro huo iliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), hukumu ya
Mahakama katika kesi iliyofunguliwa na wananchi hao ambayo Bw. Hersi Warsame Mohamed alishinda, pamoja na maelezo ya Maafisa Ardhi kutoka Manispaa ya Temeke walioshiriki katika mchakato wa maridhiano.

Utiaji saini wa makubaliano ya maridhiano hayo ulifanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu,
Magogoni, jijini Dar es Salaam, na kushuhudiwa na Walaam wa Ardhi kutoka Manispaa ya
Temeke, Bw. Salim Shedafa na Bw. Salim Urembo, pamoja na Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri
Mkuu.

Pande zote mbili zilimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan, na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa utaratibu mzuri unaofanywa
na Serikali ya Awamu ya Sita katika kutatua migogoro ya wananchi kwa njia ya mazungumzo na
maridhiano.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, kiongozi wa wananchi hao, Bw. Ivan
Kihiyo, alisema: “Tumefikia maridhiano haya kwa akili zetu wenyewe, bila kushurutishwa, na
tumekubaliana kulimaliza suala hili kwa amani. Wenzetu hawakushurutishwa na sisi
hatukushurutishwa.”

Naye Msemaji wa familia ya Bw. Hersi, Yassin Hersi Warsame, alimshukuru Mungu kwa
mgogoro huo kumalizika kwa njia ya maridhiano. Alisema familia itaendelea na uwekezaji wake
katika eneo hilo na kuchangia katika ujenzi wa Taifa la Tanzania bila bughudha.

Waziri Mkuu ameweka utaratibu wa kutatua baadhi ya migogoro mbalimbali ya wananchi
inayomfikia kupitia mikutano ya hadhara na kwa njia ya barua, kwa kutumia Kamati yake ya
Maridhiano, ambayo imeendelea kutatua migogoro mbalimbali kadiri inavyoagizwa na Waziri
Mkuu.