NA FAUZIA MUSSA

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inatarajia kufanya Kongamano la Uchumi wa Buluu kesho Agosti 12, 2026, katika eneo la Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.

Kongamano hilo linatarajiwa kuwashirikisha zaidi ya wazawa 200 kutoka pande mbili za Muungano, likiwa sehemu ya shughuli zinazofanyika katika Tamasha la Kizimkazi kwa lengo la kujadili fursa zilizopo katika Uchumi wa Buluu na namna bora ya kuzitumia kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Kapteni Hamad Bakar Hamad, alisema kongamano hilo litatoa fursa kwa wadau wa ndani kukutana na kujadili kwa pamoja namna ya kuhifadhi na kutumia kwa uendelevu vyanzo vya Uchumi wa Buluu.

Alisema mjadala huo utajikita katika masuala mbalimbali yanayohusiana na bahari na rasilimali zake, pamoja na rasilimali zinazopatikana katika mito na maziwa, ambazo zina nafasi muhimu katika kuimarisha shughuli za kiuchumi na kuongeza kipato cha wananchi.

“Kongamano hili linatarajiwa kuwa jukwaa la kujenga uelewa na kuibua mawazo yatakayosaidia kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za Uchumi wa Buluu, huku likisisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali hizo dhidi ya matumizi yasiyo endelevu,” alisema Kapteni Hamad

Alisema ushirikiano kati ya wadau wa pande mbili za Muungano ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali za majini zinalindwa na kutumiwa kwa njia endelevu, sambamba na kuweka mazingira yatakayowawezesha wananchi kunufaika na fursa zinazotokana na sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Kapteni Hamad, Uchumi wa Buluu una nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo ya wananchi kupitia shughuli mbalimbali zinazohusiana na bahari na rasilimali za majini, hivyo ni muhimu jamii kuwa na uelewa wa fursa hizo na kuzitumia ipasavyo.

Aliikumbusha jamii, hususan wazawa, kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta ya Uchumi wa Buluu katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi zinazoweza kuongeza kipato, ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

“Ni muhimu wananchi kuzitambua fursa zilizopo katika sekta hii na kuzitumia kwa njia inayozingatia uhifadhi wa mazingira na rasilimali, ili ziendelee kuwa na manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.

Aidha, alisema kongamano hilo linatarajiwa kuanza saa tatu asubuhi na kufunguliwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mboja Ramadhan Mshenga na kufungwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ng’wasi Damas Kamani.

Uchumi wa Buluu ni miongoni mwa sekta zinazotiliwa mkazo na Serikali kutokana na nafasi yake katika kuchochea shughuli za kiuchumi, hususan uvuvi, ufugaji wa viumbe maji, utalii wa baharini, usafirishaji na shughuli nyingine zinazotegemea rasilimali za bahari na maji.