Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Ziwa, Mhandisi Juma Mkobya, amesema halmashauri za Mkoa wa Mara zimetoa zabuni zenye thamani ya jumla ya zaidi ya shilingi milioni 224 kupitia Mfumo wa NeST kwa makundi ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Mhandisi Mkobya ametoa taarifa hiyo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, wakati wa kuhitimisha mbio hizo katika Mkoa wa Mara, Agosti 9, 2026, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Amesema zabuni hizo zilitolewa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, inayozitaka taasisi nunuzi kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya makundi ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, ambayo yanatambulika kama makundi maalum.
Akitaja halmashauri na thamani ya zabuni zilizotolewa, kama inavyoonekana kwenye mabano, Mhandisi Mkobya alisema ni Halmashauri ya Manispaa ya Musoma (Sh. 99,000,000), Halmashauri ya Wilaya ya Rorya (Sh. 7,400,000), Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Sh. 37,697,650), Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Sh. 55,600,000), Halmashauri ya Wilaya ya Bunda (Sh. 16,810,000) na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti (Sh. 8,000,000). Alisema halmashauri tatu hazikufanikiwa kutoa zabuni kwa makundi maalum hadi kufikia Agosti 9, 2026.
“Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, jumla ya vikundi maalum 1,590 vimesajiliwa kwenye Mfumo wa NeST katika halmashauri zote za Mkoa wa Mara hadi sasa. Makundi ya vijana ni 781, wanawake 650, wazee 91 na watu wenye ulemavu 68,” alisema Mhandisi Mkobya, akieleza kuwa Halmashauri ya Mji wa Bunda ndiyo inayoongoza kwa kusajili makundi mengi zaidi yakiwa 238.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa aliwapongeza viongozi wa halmashauri zilizopo katika Mkoa wa Mara, akizitaka kuweka nguvu zaidi katika kuhakikisha makundi yaliyosajiliwa yanapata zabuni, kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha kuwa makundi yote ya wananchi yanapata fursa ya kujiinua kiuchumi, na mojawapo ya vyanzo vya fursa hizi ni asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi inayotengwa kwa ajili ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu,” amesema Mwang’onda.
Aliongeza kuwa anaamini kupitia usimamizi wa PPRA na uzalendo wa watumishi wa umma, makundi hayo yatakuwa sehemu ya uchumi jumuishi utakaosaidia kufanikisha malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa katika Mkoa wa Mara kuanzia Agosti 1 hadi 9, 2026, na kukabidhiwa rasmi kwa Mkoa wa Mwanza.
Kikundi cha Musoma Cleaners, kilichopata zabuni katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, kiliwaambia waandishi wa habari kuwa utoaji wa zabuni kupitia Mfumo wa NeST umeleta ukombozi wa kiuchumi kwa Watanzania wote bila ubaguzi.
