Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akipokea mfano wa Hundi yenye thamani ya Shilingi Bilioni Mbili kutoka kwa Kampuni ya utoaji huduma ya simu za mkononi ya @VodacomTanzania kama sehemu ya mchango wao kwa serikali katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona nchini leo.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza baada ya kupokea mfano wa Hundi yenye thamani ya Shilingi Bilioni Mbili kutoka kwa Kampuni ya utoaji huduma ya simu za mkononi ya @VodacomTanzania kama sehemu ya mchango wao kwa serikali katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona nchini leo.
********************************
SERIKALI imetangaza watu wapya 53 ambao wameambukizwa VIRUSI vya Corona nchini na hivyo kufanya jumla ya wagonjwa kufikia 147 tangu kutajwa kwa mgonjwa wa kwanza tarehe 16/03/2020, huku Hospitali ya Rufaa ya Amana ikiagizwa rasmi kupokea wagonjwa wenye dalili ya ugonjwa wa Corona badala ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto wakati akipokea misaada kutoka katika kampuni mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona.
Waziri Ummy Mwalimu amesema kwamba katika Mkoa wa Dar es Salaam Kuna wagonjwa 38, Zanzibar 10, Mkoa wa Kagera 1, Mkoa wa Lindi 1, Mkoa wa Kilimanjaro 1, Mkoa wa Mwanza 1 na kwamba kumetokea kifo cha mtu mmoja.
“Idadi ya wagonjwa wapya 53, inafanya jumla ya Wagonjwa waliopata maambukizi ya Virusi vya Corona nchini sasa kufikia 147, watu waliopona Hadi sasa ni 11, waliofariki dunia ni 5 na Wagonjwa wote waliobaki hali zao ni nzuri,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Akizungumzia watu wanaokwenda kupata huduma za matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kuhisi kuwa na dalili za maambukizi ya virusi vya Corona, kuanzia Sasa wanapaswa kwenda kupata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Amana iliyopo jijini Dar es Salaam.
Waziri amesema watu wenye dalili wanapaswa kwenda Hospitali ya Amana kwa kuwa Muhimbili ni Hospitali ya rufaa ambayo inatoa huduma za ubingwa juu Kama vile kupandikiza vigo na upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia.
“ Kutokana na sababu hiyo, Serikali imeamua rasmi kwamba Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana ndio itatumika Kama kituo maalumu cha matibabu ya COVID -19. Lengo la Serikali ni kutaka kuilinda Hospitali ya Taifa Muhimbili, Muhimbili Kuna watu wanahitaji Upasuaji wa matibabu ya fahamu, ndani ya Muhimbili kuna watu wanahitaji matibabu ya Moyo na pia Kuna watu wanataka kupata matibabu upandikizaji wa figo, hivyo Kama tutawaacha watu waendelee kwenda Muhimbili maana yake tutakosa mahali pa kukimbilia kupata matibabu,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy ameshukuru Kampuni mbalimbali zikiwamo taasisi za Fedha kwa kutoa msaada wa Shilingi bilioni 3.2 kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona.
Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa michango ya hiyo itaelekezwa kununua vifaa Kinga kwa ajili ya Wataalamu wa Afya pamoja na kuwapatia mafunzo.
“ Kwa niaba ya Waziri Mkuu, tunawashukuru wote na nitoe wito kwa watu ambao wako tayari kuchangia , tunawakaribisha,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.