Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic Bank Tanzania, Manzi Rwegasira (kulia), akizungumza wakati wa mkutano wa Africa50, katika mjadala wenye mada “Pace Setters: African-Designed, African-Led”. Pembeni yake ni Manuel Moses, Mkurugenzi Mtendaji wa African Trade & Investment Development Insurance (ATIDI).

……….. 

Dar es Salaam, Tanzania: Afrika inapaswa kutumia zaidi mitaji yake ya ndani, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kukuza masoko ya fedha ya ndani ili kuziba pengo la ufadhili wa miundombinu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa muda mrefu, Benki ya Stanbic Tanzania imesema.

Kauli hiyo ilitolewa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu la Afrika (Africa Infrastructure Forum), lililofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, likiwakutanisha viongozi wa kisiasa, wataalamu wa masuala ya fedha na maendeleo kujadili namna taasisi za Afrika zinavyoweza kushirikiana kufadhili maendeleo ya bara, wakati ambapo uwekezaji wa kimataifa unazidi kuwa wa kuchagua.

Akizungumza katika kikao cha mjadala kilichokuwa na mada “Pace Setters: African-Designed, African-Led” (Waongoza Njia: Yaliyobuniwa na Kuongozwa na Waafrika), Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic Bank Tanzania, Manzi Rwegasira, alisema Afrika tayari ina taasisi imara za kifedha, lakini kinachohitajika sasa ni kuongeza uwezo wa taasisi hizo ili kukidhi mahitaji makubwa na yanayoongezeka ya miundombinu barani.

> “Majibu yote mazuri yatatolewa, lakini nadhani yote yanaishia kwenye suala la ukubwa. Tunahitaji kufikiria namna ya kuongeza kiwango cha kile ambacho tayari tunacho katika bara hili,” alisema Rwegasira.

Akielezea mchango wa taasisi kama Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Africa50, Rwegasira alisema taasisi hizo pekee haziwezi kugharamia mahitaji yote ya miundombinu ya Afrika.

Alisema Afrika inapaswa kuongeza uhamasishaji wa rasilimali za ndani, hususan kupitia masoko imara na yenye kina zaidi ya mitaji ya ndani, ambayo yanaweza kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya uwekezaji wa muda mrefu.

> “Tunapaswa kutumia vizuri zaidi masoko yetu ya ndani ya hati fungani za serikali. Bado ni madogo na hayana kina cha kutosha. Tunahitaji kuyakuza,” alisema.

Rwegasira pia alitaja ushirikiano wa kikanda kuwa nguzo muhimu katika kufungua vyanzo vikubwa zaidi vya mitaji, akisema nchi za Afrika zinapaswa kuacha kufanya kazi kwa kujitenga na badala yake kutumia nguvu ya pamoja ya rasilimali zilizopo barani.

> “Labda ushirikiano wa kikanda ndio mahali tunapoweza kuanzia. Tunahitaji kufanya kazi pamoja kwa ushirikiano ili kutumia mitaji tuliyonayo,” alisema.

Aliongeza kuwa mifumo bunifu ya ufadhili, ikiwemo **sekuritizasheni (securitisation)** na **urejelezaji wa mali za miundombinu (infrastructure asset recycling)**, inaweza kusaidia serikali kupata uwekezaji wa ziada bila kutegemea pekee vyanzo vipya vya mitaji.

> “Securitisation inakuruhusu kutumia tena mtaji uleule tulionao. Ikiwa tunaweza kurejeleza mali za miundombinu, tunaweza kutumia kile ambacho tayari kimejengwa kufadhili miundombinu mipya,” alisema.

Mijadala hiyo iliakisi lengo pana la jukwaa hilo la kuendeleza mfumo wa ufadhili unaoongozwa na Waafrika kupitia **New African Financial Architecture for Development (NAFAD)**, unaolenga kuunganisha nguvu za benki za Afrika, wawekezaji wa kitaasisi, kampuni za bima, taasisi za fedha za maendeleo na serikali katika kufadhili miradi ya miundombinu kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza kando ya mkutano huo, Mkuu wa Kitengo cha Corporate and Investment Banking wa Stanbic Bank Tanzania, Ester Manase, alisema jukwaa hilo limeonesha kuwa ushirikiano ni msingi muhimu katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu barani Afrika.

> “Mkutano huu umekuwa na manufaa makubwa kwetu kama benki kwa sababu umewakutanisha wadau muhimu ambao wamejikita katika kusaidia maendeleo ya miundombinu barani Afrika,” alisema Manase.

Alisema miundombinu ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi kwa kuwa hurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo na bidhaa nyingine, kuwezesha biashara ya kimataifa na kuchangia katika maendeleo ya uchumi kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Manase, somo kubwa zaidi kutoka katika mkutano huo wa siku mbili ni umuhimu wa ushirikiano kati ya benki za biashara, taasisi za fedha za maendeleo, kampuni za bima, serikali na wawekezaji binafsi, kwa kuwa hakuna taasisi moja inayoweza kugharamia mahitaji ya muda mrefu ya miundombinu ya Afrika pekee.

> “Jambo kubwa nililojifunza ni umuhimu wa ushirikiano. Kila mdau ana nafasi muhimu ya kutekeleza, lakini hakuna mmoja wetu anayeweza kufikia malengo haya peke yake,” alisema.

Manase alieleza kuwa ingawa benki za biashara zina nafasi muhimu katika ufadhili wa miundombinu, miradi hiyo inahitaji mitaji ya muda mrefu na yenye uvumilivu, ambayo inaweza kupatikana kupitia ushirikiano na taasisi za fedha za maendeleo pamoja na wawekezaji wa kitaasisi.

> “Benki za biashara zinaweza kusaidia ufadhili wa miundombinu kwa kiwango fulani. Kwa kuwa hii ni uwekezaji wa muda mrefu, tunahitaji taasisi za fedha za maendeleo, kampuni za bima, pamoja na sekta ya umma na binafsi kufanya kazi kwa pamoja,” alisema.

Mtendaji huyo pia alisema Tanzania iko katika nafasi nzuri kimkakati ya kuwa lango kuu la usafirishaji na biashara kwa Afrika Mashariki, akitaja uwekezaji unaoendelea katika bandari, reli ya Standard Gauge Railway (SGR) na miundombinu ya barabara.

> “Tanzania iko katika eneo la kimkakati sana. Tuna nchi jirani nane, ambapo sita kati ya hizo hazina bandari. Hii inatupa fursa ya kipekee ya kuwa kitovu cha ukanda huu,” alisema.

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, **Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete**, alisema ufadhili wa miundombinu unapaswa hatimaye kuboresha maisha ya wananchi na hivyo kwenda sambamba na uwekezaji katika rasilimali watu.

Dkt. Kikwete alisema ongezeko la idadi ya vijana barani Afrika linaweza kuwa faida kubwa zaidi ya kiuchumi kwa bara hilo ikiwa serikali zitawekeza katika elimu bora, ukuzaji wa ujuzi na fursa za ajira.

Alisisitiza kuwa barabara, reli na miradi ya nishati haipaswi kuonekana kama mafanikio ya maendeleo yenyewe, bali kama nyenzo za kuongeza uzalishaji, kukuza biashara na kufikia ustawi wa pamoja.