Na Mwandishi Maalum,Muleba

WAZIRI wa maliasili na Utalii ambaye ni Mlezi wa mkoa wa Kagera Mheshimiwa KIJAJI, ametembelea mradi wa ujenzi wa soko kubwa la kisasa katika mji wa Muleba na kupokelewa na wananchi .

Akiwa katika mji wa Muleba amewataka wananchi kutunza Amani ili waweze kunufaika na matunda ya uwekezaji wa serikali na kudai kuwa ikiwa wananchi hawatjivunia amani yao basi hawataweza kunufaika katika uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.

Aidha aliwatakawananchi kuhakikisha wanakuwa wa kwanza kulinda miundombinu iliyowekwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kunufaisha vizazi vingi

Amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Muleba kwa ubunifu mkubwa wa ujenzi wa soko la kisasa ambalo litapunguza adha kwa wafanyabiashara wengi ambao wanakosa maeneo mazuri ya kufanyia Biashara 

Akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Afisa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Dickson Mnyaga, amesema ujenzi wa soko hilo unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 4 katika awamu mbili. 

Amesema awamu ya kwanza yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2 imekamilika kwa asilimia 100, huku zaidi ya shilingi bilioni 1 zikiwa tayari zimetumika. Aidha, awamu ya pili itagharimu zaidi ya shilingi bilioni 1 na inatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). 

 Amesema hatua zilizosalia mpaka sasa ni uunganishaji wa umeme na uwekaji wa majina kwenye vyumba vya biashara.

Ametaja changamoto zinazoomjitokeza katika mradi huo kuwa ni ucheleweshaji wa upatikanaji wa baadhi ya vifaa vya ujenzi ambavyo havipatikani kwa urahisi ndani ya Mkoa wa Kagera, hali inayochangia kuchelewa kwa kukamilika kwa baadhi ya kazi kwa wakati.

Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba wameishukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo, hususan ujenzi wa Soko la Muleba, wakieleza kuwa mradi huo utakuwa chachu ya kukuza uchumi, kuongeza fursa za biashara na kuboresha maisha ya wananchi.