Na Silivia Amandius 

Karagwe, Kagera

Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za miradi ya maendeleo wilayani humo, huku akiomba hatua za kudumu zichukuliwe kudhibiti uvamizi wa tembo unaosababisha uharibifu wa mazao na kuhatarisha usalama wa wananchi.

Akizungumza mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), Bashungwa alisema wananchi wa kata za Rugu, Rugera, Kihanga, Nyakabanga na Nyakakika wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya uvamizi wa tembo, hivyo akaomba Serikali kujenga Kituo cha Askari wa Uhifadhi ili kuimarisha ulinzi na kupunguza madhara yanayosababishwa na wanyama hao.

Akijibu ombi hilo, Waziri Dkt. Ashatu Kijaji aliiagiza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Askari wa Uhifadhi wilayani Karagwe. Alisema Serikali imejipanga kuchukua hatua za kudumu kukabiliana na changamoto hiyo, na kwamba wananchi ambao mazao yao yameharibiwa na tembo watapatiwa kifuta jasho cha jumla ya shilingi milioni 39 ndani ya siku saba.

Katika ziara hiyo, Waziri Dkt. Ashatu pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Nyakakika na kueleza kuwa Serikali tayari imetoa shilingi milioni 250 kuanza ujenzi huo, huku shilingi milioni 250 nyingine zikitengwa kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 ili kukamilisha mradi huo.

Aidha, Bashungwa alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwawezesha wakulima wa Wilaya ya Karagwe na Mkoa wa Kagera kunufaika na zao la kahawa kupitia kuimarika kwa bei ya mazao hayo kila msimu.

Akizungumzia miundombinu, Bashungwa alisema Barabara ya Nyakahanga–Nyabiyonza–Nyakabanga–Nyakakika hadi Bweranyange yenye urefu wa kilomita 96 imepandishwa hadhi kutoka TARURA kwenda TANROADS, ambapo tayari imetengewa shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuendelea na uboreshaji wake, tofauti na awali ilipokuwa ikitengewa shilingi milioni 150 pekee.